Thursday, August 2, 2018

MFANYABIASHARA DAVIS MOSHA MIKONONI MWA POLISI BAADA YA KUWASHAMBULIA MAAFISA UHAMIAJI (Angalia VIDEO)

Baada ya kusambaa video ikimuonyesha mfanyabiashara Davis Mosha akiwapiga maafisa Uhamiaji, polisi wamemkamata mfanyabiashara huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa tuhuma hizo.

Msemaji wa idara ya Uhamiaji, Ali Mtanda amesema Mosha amewashambulia askari hao na kumnyang’anya mmoja wao simu ya mkononi baada ya kufika katika jengo la Delina lililopo Sinza Mori, jijini hapa.

"Askari walifika kwenye majengo hayo na kujitambulisha kwa mlinzi na moja kwa moja walionyeshwa ofisi za Meneja,” amesema Mtanda.

“Wakati wakifanya mazungumzo ya kikazi na Meneja huyo, ghafla akatokea Mosha na kuanza kuwafokea, kisha kuwashambulia na kumnyang'anya askari mmoja simu yake.”

Amesema alichofanya Mosha ni kinyume cha sheria ya uhamiaji namba 54 kifungu cha 45 kipengele 1F, kinachozungumzia kumzuia ofisa wa uhamiaji kufanya kazi yake ya ukaguzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo amesema tayari wamepokea taarifa ya tukio hilo, wanafanya uchunguzi kwa hatua za kisheria.

"Tunachunguza ili kujua kilichotokea ni nini, baada ya hapo ndio hatua nyingine zitafuata,” amesema Murilo.


No comments: