Thursday, August 2, 2018

BOT YAIWEKA CHINI YA USIMAMIZI MAALUMU BANK M (Angalia VIDEO)

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeisimamisha Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa Bank M na kuchukua usimamizi wa benki hiyo kutokana na benki hiyo kukosa fedha za kujiendesha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 2, Gavana wa BoT, Profesa Florence Luoga amesema BoT imechukua hatua hiyo kulinda maslahi ya wateja, wakopeshaji na wote wanaohusika na shughulia ambazo zilikuwa zikiendeshwa na benki hiyo.

“Kwa mamlaka iliyopewa BoT chini ya sheria namba 56, (1) (g,) (3) cha Sheria ya Benki ya mwaka 2006, BoT imeamua kuchukua usimamizi wa Benki M kuanzia leo tarehe 2 Agosti 2018." amesema Prof Luoga.

Prof Luoga ameendelea kusema kuwa uamuzi huu umechukuliwa baada ya kubainika benki hiyo ina upungufu mkubwa wa ukwasi kinyume na matakwa ya sheria ya kibenki na kanuni zake unaohatarisha usalama wa sekta za kifedha ambao kuendelea kutoa huduma kwa benki hiyo utahatarisha usalama wa amana za wateja wake.

Wakati huo huo BOT imesimamisha Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi mzima wa benki hiyo kuanzia leo na kumteuliwa Meneja ambaye atasimamia benki hiyo kwa kipindi chote ambacho benki hiyo itakuwa chini ya usimamizi wa BOT.

“Kutokana na uamuzi huo, BoT imeisimamisha bodi ya wakurugenzi na uongozi wa Bank M kuanzia leo, hivyo kutokana na uamuzi huo imemteua Meneja Msimamzi ambaye atakuwa na shughuli ya kusimamia benki hiyo kwa kipindi ambacho itakuwa chini usimamizi wa BoT,” amesema Luoga.

Profesa Luoga pia amesema katika muda usiozidi siku 90 kuanzia leo shuguli zote za utoaji wa huduma za kibenki katika benki hiyo zitasimamishwa ili kuipa nafasi BoT kutathimini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.

Aidha Gavana Luoga amewaondoa wasiwasi wateja wote wa benki hiyo kuhakikishia umma kuwa itendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.


No comments: