MAPISHI YA KIBANTU

Mapishi ya Mkate wa Kumimina


Mahitaji:
1.  Mchele nusu kilo
2.  Sukari robo kilo
3.  Hamira kijiko kimoja kidogo
4.  Hiliki ya kusaga nusu kijiko kikubwa
5.  Nazi moja au mbili

Jinsi ya Kupika:

Chambua mchele na kutoa mawe, kisha loweka mchele huo kwa masaa manne (4).
Kuna nazi na uichuje tui zito vikombe vitatu (3) na tui linalobaki weka kwenye bakuli.
Chukua mchele weka kwenye blenda, weka sukari, hamira na hiliki na tui zito kikombe kimoja kisha saga.

Iwapo mchanganyika utakuwa mzito hadi blenda ishindwe kusaga vizuri, ongeza kidogo tui lile uliloacha kwenye bakuli kisha saga mpaka ulainike kabisa.  Mimina kwenye sufuria safi na uache uumuke.  Ukisha umuka weka sufuria kwenye moto, chukua tui zito kikombe kingine kimoja na umimine nusu kwenye sufuria usambaze kwenye sufuria ili ukiweka unga uliousaga usipate taabu ya kuutoa mkate kwenye sufuria utakapoiva. 

Hakikisha hilo tui uliloweka chini ya sufuria linaiva na kuwa na rangi ya kahawia (brown) kisha mimina mchanganyiko wako uliosaga na usubiri kwa dakika 4.  Weka mchanganyiko wako kwenye oven na baada ya muda funua kuangalia kama mkate utakuwa umeiva, chukua kisu cha mezani au uma na ubonyeze mkate katikati, kama hakuna dalili za majimaji basi mkate utakuwa umeiva.  Chukua tena tui zito lililobaki na umimine kiasi huku unasambaza katika mkate wote na urudishe ndani ya oven kwa dakika chache na uutoe.

Chukua chombo chenye maji na kalisha sufuria ndani yake ili ipoe na uweze kuutoa mkate kwa urahisi, baada ya hapo mkate utakuwa tayari kwa kuliwa.
MKATE WAKO UKO TAYARI KULIWA. WAWEZA KUNYWEA CHAI, SODA, JUISI n.k.

Kutoka kitabu cha:
Thizila Balele Mbura (2009), Aina Mbalimbali za Mapishi, Educator Publishers, Mwanza



Mapishi ya Vitumbua
Mahitaji:
1.   Nazi moja (1)
2.   Mchele nusu kilo
3.   Sukari robo kilo
4.   Hiliki ya kusaga nusu kijiko kidogo
5.   Hamira nusu kijiko kikubwa
6.   Unga wa sembe robo kilo ugawe mara mbili, yaani moja ya nane
7.   Mafuta ya Kupikia


Jinsi ya Kupika:

Chambua mchele na uondoe mchanga na mawe kisha usafishe na uloweke kwa masaa manne (4)

Baada ya masaa manne uchuje mchele ili kuondoa maji, weka mchele kwenye blenda pamoja na sukari na tui la nazi kiasi kisha saga mpaka ulainike vizuri. 

Chukua unga wa sembe (moja ya nane) na upike uji mpaka uive (usitie sukari).  Ukishaiva uache mpaka upoe kisha uchanganye polepole na uji wa mchele (paste) uliousaga huku ukikoroga. Kisha weka  hamira na hiliki na uvichanganye vizuri katika uji huo (paste).  Mchanganyiko huo usiwe mzito sana wala mwepesi sana, uwe wa wastani.  Baada ya hapo uache uumuke.

Ukishaumuka weka kikaango chako motoni na tia mafuta kiasi kidogo kidogo katika kila shimo. Mafuta yakipata moto chota uji na uweke kwenye vishimo hivyo kisha geuza upande wa pili hadi vibadilike kuwa kahawia (brown). Pande zote zikishakuwa brown ya kutosha ipua vitumbua.
VITUMBUA VYAKO VIKO TAYARI KULIWA. WAWEZA KUNYWEA CHAI, SODA, JUISI n.k.

Kutoka kitabu cha:
Thizila Balele Mbura (2009), Aina Mbalimbali za Mapishi, Educator Publishers, Mwanza



Mapishi ya Kalimati

Mahitaji:
1.   Unga nusu kilo
2.   Sukari robo kilo
3.   Hiliki ya kusaga vijiko viwili (2) vidogo
4.   Vanila ya maji vifuniko viwili (2)
5.   Mafuta ya kupikia
6.   Nazi moja (1)
7.   Hamira kijiko kidogo kimoja (1)

Jinsi ya Kupika:

Kuna nazi na uichuje vizuri, chukua chombo chako kisafi cha kuumulia kalimati zako na uweke unga wako, weka hamira yote, weka hiliki yote, weka sukari na vanilla kisha uweke tui bubu la nazi (la kwanza) kiasi na uanze kuchanganya.  Changanya unga na mkono mpaka ulainike.  Hakikisha ukiweka tui lako usiweke jingi lisije likawa jepesi sana ukashindwa kuchota saa ya kuchoma.  Acha unga mpaka uumuke.

Unga ukishaumuka waka mafuta jikoni na yakishapata moto anza kuchoma kalimati kwa saizi utakayo hadi zitakapokuwa rangi ya kahawia (brown) zitoe motoni. KALIMATI ZAKO ZIKO TAYARI KULIWA. WAWEZA KUNYWEA CHAI, SODA, JUISI n.k.

Kutoka kitabu cha:
Thizila Balele Mbura (2009), Aina Mbalimbali za Mapishi, Educator Publishers, Mwanza

No comments: