Thursday, April 19, 2018

FATMA KARUME AIOMBA RADHI SERIKALI


Rais mpya wa Chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume ameiomba radhi serikali kwa kutoa lugha kali ambazo zilizokuwa zinaenda moja kwa moja kugusa muhimili wa Mahakama kuhusiana na mambo ambayo yanayoendelea nchini kupitia Mahakama bila ya kufuata haki za kisheria.

Fatma Karume ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar ametoa kauli hiyo jana Aprili 18, 2018 wakati akizungumza katika kipindi cha East Africa Breakfast kinachorushwa na East Africa Radio kwa njia ya simu ambapo amesema zoezi la kuteua Majaji nchini liangalie zaidi taaluma za wanaoteuliwa badala ya kuwateua kwa mrengo wa kisiasa.

"Mahakama ni muhimili unaojitegemea hivyo ni vema ukaheshimiwa kwa kuchagua Mahakimu wenye vigezo vya kitaaluma ambao watasimamia vema sheria badala ya kuyumbishwa na siasa. Mimi nipo tayari kushirikiana na serikali kwa sababu siwezi kutengeneza bajeti lakini naweza kushirikiana nao katika kuelezea mapungufu yaliyopo," amesema Fatma.

Mbali na hilo, Rais Fatma Karume ameweka wazi mipango yake ambayo anatarajia kuitekeleza katika kipindi cha uongozi wake.

"Kitu cha kwanza ni lazima tuifanye Mahakama iweze kufanya kazi zake katika weledi wake kwa hivyo watu wakiwa 'appointed' kuwa Majaji, Mahakimu tusiganye hizi 'appointed' kwa mujibu wa siasa, lazima ziwe 'professional'. Ina maana kwamba unai-Professionalize Mahakama nzima, hiyo ni 'point' namba 'one' lakini namba mbili mishahara, unajua muda mwingine tunalalamika rushwa lakini unampa mtu laki nane ayaendeshe maisha yake lakini kesi inakuja ya milioni 200 ndani yake, lazima tuweze 'ku-balance' hivi vyote ni vitu muhimu sana maana tunasema tuna muhimili wa Mahakama lakini hatuwezi kujiendesha, hivi kweli muhimili unaweza kusimama? kusimama kwa ari!! na naomba msamaha hapa sababu nasema mambo, unajua saa nyingine unakuwa na hamasa na unaweza kusema mambo ambayo yako 'emotional," amesisitiza Fatma.

Kwa upande mwingine, Fatma Karume amesema kuna madhaifu mengi katika muhimili wa Mahakama ndani ya nchi hii na katika nyanja za sheria ambapo amedai changamoto nyingine ni miundombinu mibovu ya majengo ya Mahakama.

KESI YA NONDO KUSIKILIZWA LEO 19 APRILI 2018

Kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) na Mwanafunzi wa UDSM Abdul Nondo ambayo ilipaswa kusikilizwa kwa siku mbili mfululizo kuanzia jana Aprili 18, 2018 iliahirishwa mpaka leo kutokana na Hakimu wa kesi hiyo kuwa na kesi nyingi.

Mmoja wa mawakili wa Nondo wakili Chance Mloga amesema kuwa Hakimu John Mpitanjia jana aliomba kupumzika kutokana na uwingi wa kesi alizozisikiliza siku hiyo.

Wakili huyo amesema kuwa wamekubaliana kesi hiyo kusikilizwa tena leo mapema asubuhi huku upande wa Jamhuri tayari ukiwa umeleta mashahidi wanne wa kesi hiyo.

Nondo anatuhumiwa kwa makosa mawili; Kosa la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa Ubungo na kusambaza kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.

Shtaka la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma mjini Mafinga alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha Polisi Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareto cha Mafinga.

RAIS MAGUFULI AFANYA UTEUZI WA WATU 10

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jana Aprili 18, 2018 ameteuwa watu kumi kushika nafasi mbalimbali akiwepo Prof. Idris Suleiman Kikula kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Kikula umeanza April 17, 2018.

VICHWA VYA HABARI VYA MAGAZETI YA LEO ALHAMISI 19/04/2018

Wednesday, April 18, 2018

BODI YA MIKOPO (HESLB) YATANGAZA KUANZA KUPOKEA MAOMBI KWA 2018/19


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza kuanza kupokea maombi kwa mwaka wa masomo 2018/19 kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi ujao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na bodi hiyo, mikopo hiyo itaanza kutolewa baada ya kukamilika kwa maboresho ya mfumo wa uombaji mikopo kwa njia ya mtandao.

Katika taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao (www.olas.heslb.go.tz) ambao umefanyiwa maboresho na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM).

Mkurungezi huyo alisema dirisha hilo la maombi ya mikopo litafunguliwa sambamba na kutangazwa kwa mwongozo wa kina utakaotoa utaratibu wa kuwasilisha maombi.

Pia alisema mwongozo huo utatoa utaratibu wa tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi, sifa na vigezo vitakavyotumika katika kuchambua na kutoa mikopo kwa mwaka ujao wa masomo unaotarajiwa kuanza mwezi Oktoba.

"Tunawasihi wale wote wanaotarajia kuomba mkopo wa elimu ya juu kusoma kwa makini mwongozo tutakaoutoa kwa vyombo vya habari na tovuti mwanzoni mwa mwezi Mei, 2018 na kuuzingatia," alisema.

Katika taarifa hiyo, Badru alisema kwa uzoefu wa miaka iliyopita waombaji wa mikopo waliwasilisha maombi yao bila kuzingatia mwongozo uliotolewa na kusababisha baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo.

"Mwaka jana, kwa mfano, zaidi ya waombaji 10,027 kati ya waombaji zaidi ya 61,000 hawakuambatisha nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa au hata vile vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kama tulivyoelekeza," alisema.

Alitaja nyaraka nyingine muhimu ambazo waombaji mikopo wanapaswa kuziandaa ni pamoja na nakala za vyeti vya kitaaluma za kidato cha nne, sita na stashahada ambazo zimethibitishwa na Kamishna wa Viapo - yaani wakili au hakimu.

Aidha, Badru alisema wanafunzi waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu huo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Kituo cha Afya cha Serikali.

Pia alisema wanafunzi ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya sekondari au stashahada (diploma) wawe na barua za uthibitisho wa udhamini huo kutoka katika taasisi zilizogharamia masomo yao.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa HELSB alisema mwaka huu maofisa wa bodi hiyo watatembelea mikoa mbalimbali ili kukutana na waombaji mikopo ili kuwaelimisha taratibu sahihi za kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao.

Alisema ratiba na maeneo itakapofanyia mikutano hiyo itatangazwa mwanzoni mwa mwezi Mei.

JECHA ANG'ATUKA TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR (ZEC)

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha amestaafu baada ya kumaliza muda wake wa majukumu ya tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Aprili 30, 2013 hadi Aprili 29, 2018 ambapo yeye na wajumbe wa tume hiyo wamekabidhi ripoti yao ya kazi kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.

Akitoa taarifa yake, Jecha amesema ZEC inaamini kuwa, mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa majukumu yake hasa ya uchaguzi yalitokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali na wananchi kwa jumla.

“Katika miaka mitano, ZEC imeweza kuendesha jumla ya chaguzi ndogo nne, zikiwemo tatu za udiwani na moja ya uwakilishi pamoja na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 na ule wa marudio yake Machi 20, 2016. Tume imefanya mapitio ya majimbo ya uchaguzi na kubadilisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi, majina ya majimbo na kuongeza idadi ya majimbo kutoka 50 hadi 54″, ameeleza Jecha.

“Tume imeweza kufanya uandikishaji wa wapiga kura kwa awamu mbili na kuendeleza daftari la kudumu la wapiga kura. Pia imeendesha programu mbalimbali za elimu ya wapiga kura kupitia vyombo vya habari, mikutano ya wadau, uchapishaji wa vipeperushi, majarida na makala mbalimbali”.

Pia Jecha alisema ZEC imechaguliwa kuwa kiongozi wa Uchaguzi Mkuu wa nchini Congo utakaofanyika mwezi Disemba mwaka huu.

Aidha, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ameipongeza Tume hiyo kwa kutekeleza vyema majukumu yake ndani ya miaka mitano kwa kuendesha chaguzi zote .

“Tume hii inastahili pongezi kwa kufanikisha vyema kazi waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuendesha chaguzi zote ukiwemo uchaguzi Mkuu, chaguzi ndogo na ule uchaguzi wa marudio ambazo zote hizo zilifanywa kwa ufanisi mkubwa”, amesema Dkt. Shein.

Wajumbe wa tume hiyo ambao wamemaliza muda wao ni Mwenyekiti mwenyewe Jecha Salim Jecha, Jaji Abdul-hakim Ameir Issa, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, Nassor Khamis Mohammed, Ayoub Bakari Hamad, Haji Ramadhan Haji na Salmin Senga Salmin ambao wote hao waliapishwa rasmi  Mei, 4, 2013.

WATUMISHI WA UMMA KUPATA NEEMA

SERIKALI imetangaza neema kwa watumishi wa umma 4,812 baada ya jana kubainisha kuwa kuna fursa za mafunzo 659 zitakazotolewa na Serikali ya China.

Fursa hizo za mafunzo zimejikita kwenye maeneo ya kipaumbele cha taifa yaliyoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21).

Katika mkutano wake na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari na Elimu ya Bunge mjini hapa jana, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema mafunzo yamejikita kwenye uhandisi wa viwanda, mawasiliano na usafirishaji.

Dk. Ndumbaro pia alisema mafunzo hayo yatajikita kwenye kilimo, elimu, afya, biashara na uchumi, Tehama na utawala bora.

Alisema gharama za mafunzo hayo zitagharamiwa na Serikali ya Watu wa China kuanzia usafiri wa ndege kwenda na kurudi, malazi, chakula na ada.

"Serikali, waajiri watatakiwa kuwawezesha watumishi walio chini yao kuomba na kuhudhuria mafunzo hayo kulingana na sheria, kanuni na taratibu za utumishi," alisema Dk. Ndumbaro.

WEMA, RIYAMA WAWAUMBUA WASHAKUNAKU!

WAKATI habari zikienea mitandaoni na mitaani kwamba mastaa wawili wa filamu, Wema Isaac Sepetu na Riyama Ally wako kwenye bifu, wenyewe wameibuka na kuwaumbua washakunaku na kuwaonesha kwamba wako sawa.

Awali, habari zilienea kwamba, wawili hao hawako sawa na wana bifu na hiyo ni baada ya Wema kushinda Tuzo ya Msanii Bora wa Kike kwenye Tuzo za Sinema Zetu aliyokuwa akishindania na Riyama ambapo mwanamama huyo aliangua kilio alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha runinga akisema kwamba amedhalilishwa kushindanishwa kwenye tuzo hiyo.

Kikizungumza chanzo makini kilieleza kwamba, wawili hao kwa mara ya kwanza tangu tuzo hizo zitolewe, walikutana uso kwa uso Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar ambako kulikuwa na zoezi la kumpokea msanii mwenzao, Monalisa aliyeshinda Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike Afrika huko nchini Ghana ambapo Wema na Riyama walionekana wakiwa pamoja na kuzungumza kama kawaida.

Wasanii hao walionekana kuwaumbua washakunaku waliokuwa wakisema kwamba wana bifu kwani muda mwingi walikuwa pamoja wakipiga stori na hata alipowasili Monalisa walikwenda pamoja kumpokea kwa kumkumbatia kwa pamoja kisha walichukua tuzo zake na kupiga nazo picha wakiwa wawili tu.

“Yaani Wema na Riyama wameamua kuwaumbua waliokuwa wanasema kuwa wana bifu maana walivyokutana uwanja wa ndege walionekana wakizungumza na kupiga picha pamoja na hawakuonesha kama wana tofauti yoyote,” alieleza msanii mmoja aliyekuwa uwanjani hapo aliyeomba hifadhi ya jina.

Hivi karibuni Wema alishinda tuzo mbili kwenye Tuzo za Sinema Zetu, moja ikiwa ni ya Msanii wa Kike Mwenye Ushawishi na ya pili ni ile ya Mwigizaji Bora wa Kike ambayo ilizua mjadala mzito huku wengi wakisema hakustahili kwa kuwa Riyama anaigiza vizuri kuliko yeye.

Baada ya tuzo hizo, Riyama aliangua kilio akidai kwamba alidhalilishwa kushirikishwa katika tuzo hizo na hata kama akifa ahitaji kupewa tuzo ya heshima kama wengine wafanyiwavyo.

NDALICHAKO AJITETEA RIPOTI YA CAG - Angalia VIDEO

Image result for picha ya ndalichako
DODOMA.  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe Prof. Joyce Ndalichako amesema anaitumia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kama changamoto na chachu ya kuendelea kufanya kazi nzuri.

Ndalichako ameyasema hayo jana wakati akijibu hoja za ripoti ya CAG iliyosomwa wiki iliyopita bungeni.

Wiki iliyopita mawaziri wanane walifanya mkutano na waandishi wa habari wakijibu hoja za ripoti ya CAG.

"Serikali ya awamu ya tano kwenye suala la udhibiti haina utani, kila mtu ameona kazi ambayo imefanyika, tunapopata ripoti ya CAG, inatupa chachu ya kuendelea na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya tano," amesema.

Amesema kama CAG alivyoshauri, watafanyia kazi mapendekezo ya CAG na pia watawachukulia hatua watendaji wanaotumia vibaya fedha za umma.

Ndalichako alizungumzia hoja ya CAG kuhusu ukusanyaji hafifu wa fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na akasema tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji wa madeni hayo.

"Taarifa ya CAG 2015/16 hadi 2016/17 inaonesha kuwa makusanyo yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 8 hadi bilioni 116.  Hilo ni ongezeko la asilimia 300. Takwimu hazidanganyi," amesema.

Hata hivyo amesema bado makusanyo hayo hayatoshelezi na ameitaka Menejimenti ya Bodi ya Mikopo kuhakikisha ukusanyaji wa mikopo unaimarishwa.


DIAMOND PLATNUMZ, NANDY WAKAMATWA NA POLISI

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe, amesema kuna baadhi ya wasanii ambao walianza kufanya uhuni ndani ya mitandao akiwemo mwanamuziki nyota, Diamond Platinumz,  ambaye tayari amekamatwa na polisi na anahojiwa kutokana na picha alizozungusha.

Pia Mwakyembe amesema imebidi mwanamuziki Faustina Charles ‘Nandy’ naye akamatwe kisha kuhojiwa na wanaangalia namna ya kuwapeleka mahakamani.

Image result for picha ya nandyMwakyembe ametoa wito kwa vijana kuwa mitandao si kokoro la kupeleka uchafu wote ambao umezuiwa na sheria na kwamba nchi ina utamaduni wake ambapo inahitajika kulinda kizazi cha sasa na cha kesho.

Waziri Mwakyembe amesema "Tulitunga sheria mwaka 2010 lakini tulikosa kanuni za kuweza kubana hasa maudhui upande wa mitandao, tumeshatunga hizo kanuni na sasa hivi hizo kanuni zimeanza kufanya kazi. Kuna baadhi ya wasanii wetu ambao walianza kufanya uhuni ndani ya mitandao ya kijamii jana tumeweza kumkamata msanii nyota Tanzania Diamond na tumemfikisha polisi na anahojiwa kutokana na picha chafu alizozirusha vile vile inabidi hata binti Nandy naye akamatwe ahojiwe," amesema Waziri Mwakyembe.

MWANAUME AFIKISHWA POLISI KWA KUJARIBU KUJIUA SABABU YA KUACHWA NA MKEWE


Mwanaume mmoja nchini Kenya, anashikiliwa na polisi kwa kosa la kujaribu kujiua baada ya mgogoro uliotokea baina yake na mke wake na kupelekea mkewe huyo kuamua kumuacha.

Askari Polisi wa kituo cha Migori, Gladys Rutere ameeleza kuwa mtuhumiwa, ambaye jina lake bado halijawekwa wazi kwa sababu za upelelezi alipelekwa polisi hapo na waendesha bodaboda.

Inaelezwa kuwa waendesha bodaboda hao walimkuta mwanaume huyo akijaribu kuruka kwenye daraja la mto Migori na hivyo kufanikiwa kumwokoa na baadae kumpeleka polisi.

VICHWA VYA HABARI VYA MAGAZETI YA LEO JUMATANO 18/04/2018