Thursday, May 17, 2018

ZARI: KUNA MAISHA BAADA YA KUACHANA NA DIAMOND

UKWELI ni kwamba kwenye mapenzi kuna maumivu ya namna tofauti. Kuna kuacha na kuachwa. Yanapotokea mambo hayo kwenye maisha yako, si wakati wa kuendelea kulialia kila kukicha. Nini cha kufanya? Ni kufuta machozi na kusonga mbele kwani kuna maisha baada ya hayo yote.

Zarinah Hassan Tiale, waweza kumwita Zari The Boss Lady. Ni mwanamama mburudishaji Afrika Mashariki, mjasiriamali na mama wa watoto watano ambaye anasema kwamba, licha ya kutengana na baba wa watoto wake wawili, Tiffah na Nillan ambaye ni staa wa muziki wa Afro-Pop Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, ameamua kusonga mbele maana maisha lazima yaendelee.

Wikiendi iliyopita Zari aliteka vyombo vya habari jijini Nairobi, Kenya alipohudhuria kwenye shoo aliyoalikwa kama mgeni rasmi ya Colour Purple Concert iliyolenga kutoa hamasa juu ya vita dhidi ya kansa. Mara baada ya kutua nchini humo alifanyiwa mahojiano na vituo vitatu tofauti vya runinga na kufunguka mambo mengi, ikiwemo ishu ya kuachana na Diamond. Hapa tunakuletea baadhi ya maswali na majibu ambayo yamekuwa yakiulizwa kwenye mitandao ya kijamii bila yeye mwenyewe kuyajibu, lakini sasa yamepata majibu.
Swali: Kwa asiyekufahamu, Zari ni nani?
Zari: Mkurugenzi wa Vyuo vya Brooklyn (vipo Afrika Kusini), mwanamke jasiri, mama wa watoto watano na mwanamke anayewashawishi vijana wadogo kujitambua na kuwa watu fulani kwenye jamii.

Swali: Umesema ni mama wa watoto watano, lakini tunajua unalea mwenyewe bila baba zao, je, huwa unapata wapi sapoti?

Zari: Ni kweli sina sapoti ya baba zao, naamini wengi wanajua kilichotokea kwa baba zao. Napata sapoti kutoka kwa ndugu zangu, kaka na dada zangu. Pia kuna mtu anaitwa Kinje (mtoto wa mzee Kingunge) kutoka Tanzania. Mara nyingi huwa ninamtegemea na likitokea lolote ananishauri juu ya familia.

Swali: Mara nyingi tunaona picha zako ukiwa na wanao kwenye mitandao ya kijamii, je, huwa unawafundisha nini?

Jibu: Kwa wa kiume, maana ninao wanne, ninawafundisha kuwa na heshima na hasa kuwaheshimu wanawake. Tiffah yeye ni mwanamke wa kipekee. Huwa ninamjenga kuwa mwanamke kamili kwa kujiamini na kuwa imara. Anapenda kupika, ninamjengea mazingira ya kuwa mwanamke kamili.

Swali: Je, wanachukuliaje maisha yako ya mitandaoni hasa wanapoona unatukanwa na mambo mengine kama hayo?

Zari: Wale wanajua, kuna Zari wa mitandaoni na kuna mama yao ambaye ni mtu tofauti kabisa na yule wa mitandao ya kijamii.
Swali: Wengi tunaweza kuwa hatujui, ni nini hasa kilikufanya uachane na Diamond?
Zari: Wanawake wengi wanakutana na mambo ya ajabu kwenye uhusiano, lakini wanaogopa kutoka. Wengine wanaamini wakiwa wenyewe hawawezi. Kweli nilimpenda sana (Diamond) na nilikuwa tayari kwa lolote, lakini sipendi mtu anikosee heshima. Angeweza kufanya mambo yake yote ya kutembea na wanawake wote, lakini aniheshimu. Alizidisha kutoniheshimu. Mimi ninapenda kuheshimiwa. Bila yeye, mimi nasonga mbele kwa sababu bado kuna maisha.

Swali: Umefuata nini Kenya?Zari: Napenda kusaidia jamii, nipo hapa kuhamasisha watu hasa mabinti wadogo kujua vita dhidi ya kansa. Unajua watu wengi hawajui, lakini mama yangu (Halima Hassan) alikufa kwa kansa. Ilichelewa sana kugundulika. Kilichogundulika mapema ilikuwa ni kisukari na presha, lakini baadaye madaktari ndipo waligundua ana kansa ambayo ilikuwa imefikia kwenye ngazi mbaya. Nilimwona mama yangu alivyokuwa akiteseka kwa sababu ukimuona mama yangu unakuwa umeniona mimi. Hivyo ndiyo maana huwa ninahamasisha vita ya kansa.
Swali: Umekumbusha kipindi kile ulipofiwa na mama yako yalisemwa mengi ikiwemo wewe kutolia, je, ilikuwaje?
Zari: Unajua mimi nilikuwa ndiye kila kitu na kila mmoja wakiwemo wanangu walitegemea sana uimara wangu. Kama nilivyosema, mama yangu alikuwa ameteseka sana. Kutokana na hali yake ilivyokuwa, nilikuwa nimejiandaa kisaikolojia ndiyo maana sikulia. Pia nilikuwa nimeshalia sana maana nilijua kilichokuwa kinakuja mbele yangu.
Usisahau mama yangu alifariki dunia wiki saba tu baada ya Ivan (aliyekuwa mumewe kabla ya Diamond) kufariki dunia. Na wakati huohuo nilikuwa kwenye matatizo na x wangu (Diamond) kutokana na ku-cheat (kusaliti) na mwanamke mwingine (Hamisa Mobetto). Ilikuwa kama kuna mtu ameamua kunipiga makofi kwelikweli, yaani ukigeuka huku unasikia paa…ukigeuka huku unasikia paa…

Swali: Tunajua kwenu ni Uganda, je, Afrika Kusini unaishi wapi? Na je, ni kwako?
Zari: Yeah…kwetu ni Uganda, lakini nimekuwa nikiishi Afrika Kusini huu ni mwaka wa 18. Na kule ninaishi nyumbani kwangu jijini Pretoria. Ni mji mzuri wa kibiashara na kitalii. Pako vizuri sana, ninapapenda.

Swali: Kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa na maneno mengi juu ya umri wako huku kila mtu akitaja wa kwake, je, una umri wa miaka mingapi?
Zari: Nina umri wa miaka 37 na mwaka huu ninatimiza umri wa miaka 38. Kuna wengine huwa wanasema nina miaka 45, lakini hata wangesema nina miaka 100 hakuna shida ilimradi tu mimi ninajielewa.

Swali: Zari una kila kitu kwa maana ya utajiri, magari na nyumba, je, unatamani kuwa na nini tena maishani mwako?
Zari: Private jet (ndege binafsi)…yees…private jet na ni lazima niwe nayo kwa sababu nipo kwenye mipango hiyo.

Swali: Baada ya kuachana na Diamond mwanaume wako kwa sasa ni nani?
Zari: Ni kweli mimi ni mwanamke mzuri, mwanamke wa mfano, nina kila kitu anachohitaji mwanaume na ni mwanamke anayejua future (maisha ya baadaye) hivyo kila mwanaume angetamani kuwa na mimi. Lakini kwa sasa sina, ninahitaji kupumzika kwanza na nipo huru sana. Ni kweli kuna foleni ndefu ya wanaume wanaonitaka, lakini mimi sihitaji. Nawaangalia watoto wangu kwanza, nataka litakapotokea la kutokea niwaachie kitu cha kujivunia na siyo wateseke. Halafu pia nikiwa na mwanaume lazima itajulikana tu maana mimi ni maarufu kwa hiyo ataonekana kila mahali kwenye mitandao ya kijamii.


No comments: