Tuesday, March 6, 2018

WANAHARAKATI WAKERWA NA KAULI YA DK KIGWANGALLA

Dar es Salaam. Makundi ya kutetea haki za binadamu yamelaani kauli iliyotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla kuhusu kuzamishwa mitumbwi ya raia wa kigeni inayoingia kwenye Pori la Akiba la Kimisi na Burigi mkoani Kagera ili warejee walikotoka wakiogelea.

Mwishoni mwa wiki, Dk Kigwangalla alikaririwa akisema kuzamishwa kwa mitumbwi hiyo ni kama kutuma salamu kwa wanaoingia nchini kwamba, Tanzania si shamba la bibi, bali nchi ya watu inayopaswa kuheshimiwa, Mapori hayo pamoja na la Biharamulo yanatenganishwa na Mto Kagera na nchi ya Rwanda.

Wakionyesha kuchukizwa na maelekezo ya waziri huyo, wanaharakati waliozungumza na waandishi wetu jana walisema Dk Kigwangalla anapaswa kuomba radhi na kutengua kauli yake kwa kuwa inawafundisha wananchi kuanza kuchukua sheria mikononi.

“Hii ni kauli ya hatari kutoka kwa kiongozi na tena ni makosa makubwa kuwahimiza wananchi wafanye kitendo hicho... kama kuna wakosaji, sheria inapaswa kufuatwa,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba.

Alisema Tanzania ni nchi yenye vyombo vya ulinzi na usalama, hivyo kama kunajitokeza vitendo vinavyokwenda kinyume cha sheria, basi vyombo husika vinapaswa kushughulikia na si kutoa matamko ya namna hiyo.

Dk Kijo Bisimba alisema ingawa hoja za Dk Kigwangalla ni za msingi kuhusu kulinda rasilimali za Taifa, lakini haikubaliki kwa kiongozi kama yeye kutoa matamshi yanayoweza kuhatarisha usalama wa raia wa nchi nyingine.

“Raia hapaswi kupoteza maisha kwa jambo lolote lile labda kama ni vita, na hata kama wao wanatufanyia sisi jambo baya; hatupaswi kufanya hivyo. Watu waachwe wafanye shughuli zao za kijamii na sheria za nchi zifuatwe,” alisema.

Hoja kutaka kufuatwa kwa sheria za nchi iliungwa ilitolewa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron Mwakagenda aliyesema nchi haiwezi kuendeshwa kwa matamko kama hayo.

“Waziri lazima aombe radhi, lazima sheria zifuatwe, hatuwezi kuendesha mambo kwa matamko ya Dk Kigwangalla,” alisema.

Alisema matamshi kama hayo yanaweza kusababisha kuvuruga na hata kuzorotesha uhusiano baina ya nchi akitoa mfano wa namna Tanzania na Kenya zilivyowahi kutumbukia katika mvutano wa kibiashara kutokana na matamko yaliyokuwa yakitolewa.

“Unakumbuka namna Tanzania na Kenya zilivyoingia kwenye mzozo wa kibiashara na kuleta mtafaruku. Hatutaki kuona haya mambo yakijirudia,” alisema.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya waliwaagiza mawaziri kushughulikia kero zinazokwamisha ufanisi wa kibiashara na kutaka changamoto hizo zitatuliwe mara moja.

Tanzania imewahi kuingia kwenye mvutano wa kibiashara na Kenya baada ya kushuhudiwa matukio kadhaa yakiwamo yaliyohusisha uchomaji moto vifaranga vya kuku vilivyoingizwa nchini pasipo kufuata taratibu.

Kwa mtazamo wake, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema Waziri Kigwangalla anatakiwa kujua kwamba Taifa linaongozwa kwa utawala wa sheria na si hisia au mihemko ya mtu.

Alisema kauli ya waziri huyo inajenga uhasama na uadui, “Viongozi waache kuhamasisha watu kujichukulia sheria mkononi,” alisema.

Alisema mtandao huo unaojishughulisha na masuala ya haki za binadamu umekuwa ukipinga vitendo hivyo mara kwa mara, huku ripoti zikionyesha kila mwaka watu zaidi ya 1,000 wanapoteza maisha kwa watu kujichukulia sheria mkononi.

Olengurumwa alisema Taifa linaendelewa kwa kufuata utaratibu na iwapo kuna mtu amekosa taratibu zifuatwe, Mratibu huyo ambaye pia ni mwanasheria alisema chini ya sheria, mtu yeyote anachukuliwa hajatenda kosa mpaka pale mahakama itakapothibitisha kwa kuwa ndicho chombo cha mwisho cha kutoa haki.

“Tunalaani kauli hizi zinazokwenda kinyume cha haki za binadamu, utawala wa sheria, masuala ya utawala bora na mahusiano ya kidiplomasia,” alisema.

No comments: