Friday, November 24, 2017

TANZIA: MBUNGE WA SONGEA MJINI, LEONIDAS GAMA AFARIKI DUNIA

Marehemu Mhe. Leonidas Gama enzi za uhai wake.

Mbunge wa Songea Mjini, mkoani Ruvuma, Mhe. Leonidas Gama amefariki dunia usiku wa kuamkia leo 24 Novemba, 2017 akipatiwa matibabu katika hospitali ya Peramiho iliyopo mkoani humo.

Mheshimiwa Gama kabla ya kuwa Mbunge amewahi kushika nyadhifa nyingine za kiserikali ikiwemo Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro wakati wa utawala wa awamu ya Nne. Bunge limethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baadaye.

Taarifa za kifo chake zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii mapema leo asubuhi ambapo marafiki zake wa karibu na marehemu, akiwemo diwani wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Mhe. Songoro Mnyonge ameandika katika ukurasa wake wa Facebook, akieleza kusikitishwa kwake na kwamba taarifa za kifo cha Mbunge huyo amezipokea majira ya saa 7 usiku wa kuamkia leo Novemba 24, 2017.

Katika maandishi yake Mhe. Mnyonge alieleza masikitiko yake kwani ni wiki tatu tu Mhe. Gama alimpigia simu na walijadiliana kuhusu matibabu ya nduguye, Dominic Gama ambaye anapatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.
Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Leonidas Gama akipimwa afya na Muuguzi Asha Shao bungeni Dodoma.
Katika picha hii ya maktaba, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akimuapisha Mhe. Leonidas Gama kuwa Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.
Katika picha hii ya maktaba Mhe. Waziri Mkuu, akizungumza jambo na Mhe. Leonidas Gama, Mbunge wa Songea mjini, kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Mhe. Leonidas Gama akiwa na wabunge wenzake, Mhe. Hamisi Kigwangalla, (mbunge wa Nzega), na Mhe. Sixtus Mapunda, Mbunge wa Mbinga mjini.
Katika picha hii ya maktaba, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe.Leonidas Gama akisalimiana na viongozi wa wilaya ya Rombo mara baada ya kuwasili katika shule ya sekondari Olele kwa ziara ya kikazi.

No comments: