Saturday, November 18, 2017

DAKTARI ADAKWA RUSHWA YA 150,000/-

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro, inamshikilia Dk. Deogratius Urio wa Hospitali ya Rufani ya Mawenzi kwa tuhuma za kudai na kupokea rushwa ya Sh. 150,000.

 Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa katika vyombo vya habari na Takukuru, Dk. Urio alikamatwa jana akiwa kwenye baa maarufu ya Mombasa High Way iliyoko Himo baada ya kuwekewa mtego na makachero wa Takukuru.

Taarifa hiyo ambayo ilitiwa saini na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, ilieleza kuwa kukamatwa kwa daktari huyo kunatokana na malalamiko ya ndugu wa mgonjwa aliyekuwa akizungushwa kufanyiwa upasuaji.

Makungu alisema mgonjwa huyo alikuwa akihitaji kufanyiwa upasuaji wa uvimbe katika kizazi tangu Oktoba, mwaka huu, baada ya kufanyiwa vipimo kwenye hospitali hiyo na kubainika kuwa na tatizo hilo.

 “Licha ya kubainika kuwapo na uvimbe huo mgonjwa huyo hakupata tiba haraka baada ya kuelezwa na daktari huyo kuwa hawezi kufanyiwa upasuaji hadi hapo atakapotoa fedha hizo,”alisema.

Makungu alisema baada ya kupata taarifa hizo, waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata  Novemba 15, mwaka huu, akiwa kwenye  baa hiyo.

Alisema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo na utakapokamilika, atafikishwa mahakamani.

 “Takukuru inatoa rai kwa madaktari na wauguzi katika hospitali ya Mawezi kuzingatia viapo vyao ili Mawenzi iwe hospitali ya kuigwa kwa huduma bora,” alisema Makungu.

 Aidha, alitoa rai kwa wote ambao watakiuka viapo vya maadili ya kazi zao na kuonya kuwa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

No comments: