Wednesday, November 15, 2017

TAMKO ZITO FAO LA KUJITOA

Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


BUNGE limezima mjadala wa fao la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii bungeni baada ya jana, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kutoa tamko zito likifafanua bayana kuwa tayari nchi ina sheria iliyofuta fao hilo.

Dk. Tulia alitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu mwongozo ulioombwa kwake na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), kuhusu fao hilo baada ya serikali kueleza bungeni jana kuwa bado inalifanyia kazi. Mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo nchini ni pamoja na NSSF, PSPF, GEPF, PPF na LAPF.

Katika kujenga hoja yake, Waitara alisema kuwa wakati Ofisi ya Waziri inajibu swali bungeni kuhusu suala hilo jana asubuhi, ilisema mchakato wa fao la kujitoa unaendelea kufanyika na kwamba, uamuzi wake haujafanyika.

"Jambo hili limekuwa na mkanganyiko mkubwa sana,” alisema Waitara na kuongeza:

“Wapo watu waliostaafu kazi hawajapewa mafao yao, wapo watumishi ambao wanafanya kazi kwa mkataba, mkataba ukiisha anaambiwa mafao yako usubiri mpaka ukifikia umri wa miaka 55.

"Wapo watu wanafanya kazi katika mazingira magumu, wanataka waache kazi wapate mafao yao waanzishe shughuli mbalimbali za maendeleo kulingana na kipato, waweze kujikimu.

"Na wapo watu ambao kimsingi Mheshimiwa Naibu Spika, ni wagonjwa…wanahitaji mafao yao ili wajitibu na wasomeshe watoto wao. Hili zoezi limeshindikana.

"Sasa naomba mwongozo wako kwa sababu kama Naibu Waziri anasema kwamba jambo hilo lipo kwenye mchakato na wabunge wanaulizwa na wananchi wao kwa nini hawapewi fedha zao, wanaambiwa serikali imeelekeza mpaka ufikishe miaka 55."

Waitara alidai sheria hiyo hajawahi kuiona, mjadala haujawahi kufanyika na kwamba, jambo hilo halijawahi kupitishwa na bunge.

Alishauri wafanyakazi waendelee kupata haki zao na kama kuna mchakato, kauli ya serikali itoke ili wapate haki zao mafao yao
yawasaidie kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.

"Mchakato utakapokamilika kwa ujumla wake, Watanzania watapata maelezo mengine. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwongozo wako katika jambo hili muhimu sana," alisema.

Akijibu mwongozo huo, Dk. Tulia ambaye jana aliongoza kikao cha Bunge kwa mara ya kwanza tangu mkutano wa tisa wa Bunge la 11 lianze Jumanne ya wiki iliyopita, alisema kuna sheria iliyofuta fao la kujitoa na iliwasilishwa bungeni na kuridhiwa na chombo hicho cha kutunga sheria.

"Waheshimiwa wabunge, huu mchakato ulianza muda mrefu na hata hapa bungeni sheria iliwahi kuletwa… sheria ilishatungwa. Na mpaka sasa tunapozungumza sheria ya mwisho kabisa iliyopitishwa na Bunge hili inakataza fao la kujitoa," Dk. Tulia alisema.

"Kwa hiyo, mchakato maana yake ni mazungumzo sasa ya kuangalia namna ya kubadilisha tulikotoka, lakini sheria iliyopo mpaka ninapozungumza inakataza fao la kujitoa."

Dk. Tulia aliongeza kuwa mifuko ya hifadhi za jamii imeweka utaratibu wa ziada ukiacha yale mafao ambayo yako kisheria.
Alisema utaratibu huo unaipa mifuko huo fursa ya kuamua kujitengenezea utaratibu, lakini sheria iliyopitishwa na bunge inakataza fao la kujitoa.

 "Kwa hiyo, mwongozo wangu katika hilo, kwamba mchakato gani unaendelea, ni kwamba sheria tunayo tayari," Naibu Spika huyo alisema, "kama kuna mchakato unaendelea basi pengine ni wa mazungumzo kati ya serikali na wafanyakazi na waajiri kuona namna bora ya kulifanya hilo jambo.

"Na mimi nadhani kwa namna lile swali lilivyokuwa limeulizwa, ni vizuri kujiridhisha na tafiti zilizofanywa kuhusu fao la kujitoa kama ni jambo ambalo kama nchi ambao tumesaini mikataba mbalimbali kuhusu wafanyakazi, kuhusu waajiri na serikali, ni jambo ambalo tunataka kuliendea?

"Kwa hiyo, kama kuna mchakato wowote ambao unaendelea serikalini, basi mfanye haraka ili tuseme tunasimama wapi."

Awali, hoja ya fao la kujitoa iliibuka asubuhi wakati wa kipindi cha maswali baada ya Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Sonia Jumaa Magogo, kutaka kauli ya serikali kuhusiana na fao hilo.

Akijibu swali hilo la nyongeza, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia vijana na ajira, Antony Mavunde, alisema serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo ikishirikiana na wadau kuona njia bora ya kutatua changamoto zinazojitokeza kwa wadau wote.

Katika swali lake la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mkakati gani dhidi ya waajiri ambao hawaandikishi watumishi wao katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kuwasababishia kukosa stahiki zao.

Katika majibu yake kuhusu swali hilo, Mavunde alisema mkakati wa serikali katika kuhakikisha waajiri wote wanaandikisha wafanyakazi wao ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii Na. 8 ya mwaka 2008 kifungu cha 30.

Alisema kifungu hicho kimeweka utaratibu unaomtaka mwajiri kuwaandikisha watumishi wake katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

"Mwajiri anayekiuka matakwa ya kifungu hicho anastahili adhabu ya kulipa faini ya kiasi kisichozidi Sh. milioni 20 kwa mujibu wa kifungu cha 55 cha Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii," alisema Mavunde.

Aliongeza kuwa katika kuimarisha usimamizi wa sheria za kazi, serikali kupitia Bunge ilifanya marekebisho ya Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya mwaka 2004 ili adhabu ya papo kwa papo itolewe kwa waajiri wanaokiuka matakwa ya sheria ikiwa ni pamoja na kutosajili wafanyakazi katika mifuko ya jamii.

No comments: