Saturday, November 18, 2017

RUNGU LAJA KUDHIBITI KODI TATA ZA NYUMBA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula.

SERIKALI imesema iko mbioni kukamilisha mwongozo utakaowezesha wapangaji wa nyumba nchini kulipa pango la nyumba kwa mwezi mmoja mmoja badala ya miezi sita au 12 inavyofanyika sasa kwa wamiliki wa nyumba za biashara nchini.
   
Pia imeweka wazi kuwa inatarajia kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Nyumba itakayohakikisha mwongozo huo unatekelezwa kikamilifu ili kukomesha ilichokiita uonevu unaofanywa na wamiliki wa nyumba kwa wapangaji.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, ndiye alitoa kauli hiyo bungeni mjini hapa jana alipokuwa anajibu swali la nyongeza la Halima Bulembo.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) alitaka kujua kwanini serikali haioni haja ya kudhibiti upandaji holela wa pango la nyumba ambao unaathiri wananchi wengi kutokana na kipato chao kuwa duni.

Katika majibu yake, Mabula alisema tayari mchakato wa kuanzisha mamlaka umeshakamilika na muda mfupi ujao wapangaji wataanza kulipa kodi kwa mwezi mmoja mmoja.

"Serikali italeta mwongozo huo humu bungeni ili waheshimiwa mpate muda wa kuupitia na kuupitisha," alisema Mabula.

Katika swali lake la msingi, Bulembo alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kudhibiti upandaji holela wa gharama za pango kwa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Akijibu swali hilo, Mabula alisema utaratibu wa kurekebisha viwango vya kodi ya nyumba za NHC husimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi ambayo imepewa mamlaka ya kisheria ya kusimamia kodi ya pango pamoja na kuidhinisha viwango vya kodi vinavyotozwa kwa wapangaji wa nyumba za shirika.

“Utaratibu wa kupandisha kodi kwa sasa hufanyika pale mkataba wa mpangaji unapomalizika na mpangaji kuomba kuhuisha makataba wake. Ieleweke kuwa kodi zinapanda kwa mujibu wa sheria pale mkataba wa mpangaji unapomalizika muda wake,” alisema Naibu Waziri huyo.

No comments: