Saturday, November 18, 2017

MASHAHIDI 33 WASALIA KUAMUA KESI YA MAUAJI YA BILIONEA MSUYA

MASHAHIDI 33 waliosalia kuijenga kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara tajiri wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya (43) wataisubirisha Mahakama Kuu, kanda ya Moshi hadi mwaka ujao kutokana na ratiba ya vikao vya usikilizaji wa kesi hiyo kufikia ukomo jana.

Kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2014, inayosikilizwa na Jaji Salma Maghimbi, kwa wiki tano mfululizo, ameshasikiliza mashahidi saba wa upande wa mashtaka na mashahidi wawili katika kesi ndani ya kesi kuanzia Oktoba 16 hadi Novemba 17, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Bernard Mpepo, imeeleza kuwa sababu za kuahirisha usikilizaji wa kesi hiyo ni kutokana na ratiba iliyopangwa kufikia ukomo, kusubiri hadi mwakani, tarehe na siku itakayopangwa tena.

“Jaji (Maghimbi) ameahirisha kesi hiyo ili kutoa fursa kwa upande wa mashtaka kujipanga upya kutafuta mashahidi wengine waliosalia, ingawa pia, ratiba yake ya kusikiliza kesi hiyo kwa mwaka huu ilikuwa imefikia mwisho. Sasa itasubiri kuendelea na usikilizwaji wake tarehe na mwezi mwingine ambayo utakaopangwa na mahakama mwaka ujao.”

Kabla ya kuahirisha kesi hiyo jana, Jaji Maghimbi alisikiliza ushahidi uliotolewa na Mchunguzi wa Polisi aliyebobea katika masuala ya kielektroniki na takwimu za kielekroniki kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Inspekta William Mziu.

Shahidi huyo ni mbobezi mwenye zaidi ya vyeti 10 vya taaluma zaidi ya 10 ambavyo baadhi yake vimo vya taaluma za kiuchunguzi kama Forensic Investigation (uchunguzi wa kina wa kijinai), Mobile Forensic (uchunguzi wa simu), Computer Forensic (uchunguzi wa kompyuta), Digital Crime Management (uchunguzi wa masuala ya uhalifu katika utawala) ambavyo alisoma Israel, Mauritius na India na ana shahada ya kwanza ya elimu.

Kwa mujibu wa Msajili huyo, mashahidi 16 kati ya 49 wanaoijenga kesi hiyo, tayari wameshatoa ushahidi wao mahakamani hapo na ambao wamesalia kutoa ushahidi ni 33.

Februari 10, mwaka huu, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula, ulidai mahakamani hapo kwamba unakusudia kuleta mashahidi hao na vielelezo 40 ikiwamo bunduki moja aina ya SMG inayodaiwa kutumika kuondoa uhai wa Bilionea Msuya.

Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi 22, Agosti 7, mwaka 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, Kando kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Sharif Athuman (31), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Saidi maarufu kama “Mredii” (38), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na Mussa Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu

Wengine ni Jalila Said (28), mkazi wa Babati, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, Wilaya ya Siha, Sadiki Jabir a.k.a “Msudani” (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, Wilaya ya Hai, na Alli Musa maarufu “Majeshi”, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, unaongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdala Chavula.  

Jopo la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo linaongozwa na wakili Hudson Ndusyepo anayemtetea mshitakiwa wa kwanza, Majura Magafu anayemtetea mshitakiwa wa pili na wa tano, Wakili Emmanuel Safari anayemtetea mshitakiwa wa tatu na John Lundu anayemtetea mshitakiwa wanne, sita na saba.

Hadi sasa, mashahidi 16 wa upande wa mashtaka, wameshatoa ushahidi wao mahakamani hapo akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Upepelezi wa Wilaya ya Hai, (OC-CID) Joash Yohana, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai (DMO) Dk. Paul Chaote (39) na Khalid Sankamula (49) ambaye ni Mganga wa Kienyeji na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Limbula, Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora.

Wengine ni Anase Khalid (37), mkulima na mkazi wa Kaliua, Tabora, Mbazi Steven (32), mkazi wa Arusha na Ofisa Upelelezi, Kitengo cha Intelijensia ya Jinai mkoa wa Kilimanjaro, Herman Ngurukisi (40), Inspekta Samueli Maimu (45) ambaye alikuwa kiongozi wa timu ya ufuatiliaji ya Polisi (CRT) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa mkoa wa Kilimanjaro.

Wamo pia Ofisa Upelelezi (Detective) Sajenti Atway Omari aliyekuwa katika timu ya CRT, mtaalamu wa makosa ya kimtandao wa ofisi ya RCO, Detective Koplo Seleman Mwaipopo na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Moshi Mjini, Poncian Claud, ambaye ni mlinzi wa amani.

Wengine ni Elirehema Msuya maarufu ‘Kakaa’ ambaye ni dereva wa Hoteli ya SG Resort ya Arusha na Karim Mruma, dereva binafsi wa marehemu Bilionea Msuya na  Inspekta mziu.

No comments: