Wednesday, September 20, 2017

WANANCHI WASUSIA MKUTANO WA RC MBEYA


WANANCHI wilayani Kyela mkoani Mbeya wamesusia kuhudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, kwa madai tangu aitishe mikutano ya kusikiliza kero zinazowakumba hakuna hata moja iliyopata ufumbuzi.

Makalla alifanya ziara ya siku moja juzi wilayani humo, ambapo alikagua ujenzi wa barabara kutoka Kikusya-Matema inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na baada ya hapo alikwenda uwanja wa Siasa kwa ajili ya mkutano wa kusikiliza na kujibu kero za wananchi.

Baada ya kufika uwanjani akiongozana na viongozi wa mkoa na wilaya na kushuhudia idadi ndogo ya watu, aliondoka ghafla kurejea mkoani.

Joshua Ngalya, mkazi wa Kyela, alisema Makalla aliamua kuondoka baada ya kuona uwanja hauna watu licha ya gari la matangazo kutangaza siku mbili kabla uwapo wa mkutano huo.

Sanke Josphat, mkazi wa Kyela, alisema wakazi wa Kyela walisusa kuhudhuria mkutano huo baada ya awali kuzungumza nao ambapo wananchi walitoa kero zao ambazo ziliahidiwa kutatuliwa pasipo kutatuliwa.

Alisema wilaya ya Kyela licha ya kuwa na vyanzo vingi vya mapato, inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimekosa ufumbuzi licha ya mkuu wa mkoa kuanza kuitisha mikutano kusikiliza kero huku wataalama wakizijibu, lakini hazijapatiwa tiba.

Isakwisa Kijambile, mkazi mwingine wa Kyela, alisema mikutano inafanyika mara kwa mara na wao wanatoa kero nyingi lakini hutupwa kapuni.

Alitaja kero hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa soko la uhakika la kakao na kutokuwa na bodi ya kusimamia, hivyo makampuni yanayonunua yanaminya mizani na kuwanyonya.

Alisema pia Kyela kuna miradi iliyotelekezwa kama soko la kimataifa la kilimo lililopo Kafundo, kata ya Ipinda ambapo zaidi ya Sh. milioni 400 zimetumika kwenye jengo, lakini limegeuka makazi ya ngedere.

Alisema katika jengo la kilimo na mifugo la kata ya Talatala, zaidi ya Sh. milioni 300 zimetumika kulijenga lakini limetelekezwa.

“Ndugu mwandishi hapa tutatoa kero gani ili tusikilizwe, wakati tumetoa kero nyingi hazina majibu, ni bora tuendelee na shughuli zetu za uzalishaji mali kuliko tuache kazi twende kusikiliza na kutoa kero ambazo tunajua wazi hazitafanyiwa kazi,” alisema Kijambile.

No comments: