Tuesday, November 18, 2014

SANGOMA AZIMIA AKITOA MAJINI

Sangoma akiwa hoi baada ya kushambuliwa.
INASHANGAZA sana! Katika hali isiyokuwa ya kawaida mganga wa kienyeji ‘sangoma’ mmoja aliyefahamika kwa jina la Lambalamba amejikuta akiingia kwenye hatua ya nusu kifo kufuatia kupoteza fahamu baada ya kuelemewa na majini aliyokuwa akiyatoa shuleni. 

Tukio hilo la aina yake lilijiri hivi karibuni maeneo ya Kiluvya - Madukani jijini Dar es Salaam kwenye Shule ya Msingi Makurunge ambapo sangoma huyo aliitwa kuyatoa majini yaliyokuwa yakiwafanyia mauzauza wanafunzi na walimu.

ILIVYOKUWA
Kwa mujibu wa shuhuda mmoja wa tukio hilo, wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakisikia sauti za ajabuajabu shuleni hapo hali iliyokuwa ikiwafanya wasome kwa hofu. “Hali hiyo ilipozidi baadhi ya wanafunzi wakaenda kuwaambia wazazi wao ambao nao walipopeleleza kwa baadhi ya walimu walihakikishiwa kwamba ni kweli shuleni hapo kuna majini yanawasumbua wanafunzi na walimu pia,” alisema shuhuda huyo.

Ili kuwanusuru wanafunzi kutoka kwenye mauzauza hayo, wazazi waliweka kikao cha dharura na kuamua kuandika barua kwenye ofisi za serikali ya mtaa ili kuomba kibali cha kuitwa sangoma mkali, mwenye sifa, anayejua majini, afike shuleni hapo kuyafukuza.

Ilidaiwa kuwa mauzauza ya shuleni hapo ni wanafunzi wakienda chooni husikia vilio vya watoto wachanga au paka lakini hawaonekani. Wakati mwingine hupatwa na hali isiyoweza kuelezewa kwa lugha sahihi.

SANGOMA ATINGA
Ikazidi kudaiwa kuwa, serikali ya mtaa japokuwa haiamini ushirikina, iliwaruhusu wazazi hao kutekeleza azma yao lakini serikali isihusike kwa lolote litakalotokea. Siku ilifika, sangoma huyo akaitwa, akiwa na wasaidizi wake wawili, alitia timu kwenye eneo hilo na kujigamba kuwa, tabu ya majini imekwisha!  Yeye ndiye Lambalamba bwana!
Sangoma mwenye usongo (scalf) mwekundu akiingia kazini na timu yake kutuliza majini.
ATAKIWA MBUZI MNONO 
Habari zinasema kuwa, ili kazi ifanyike kwa ufanisi na kuweza kuleta tija na ili wanafunzi hao wampe tano kwa kazi, sangoma huyo alitaka mbuzi mnono kwa ajili ya kumchinja ili damu yake imwagikie eneo hilo na majini kukimbia.

Mbuzi alifikishwa, maandalizi ya uchinjaji yakafuatia huku sangoma akianza kusema maneno ya ‘kitaalamu’ kuashiria kuwa sasa kazi imeanza, majini yakae tayari kwa kukimbia eneo la shule.
Timu hiyo ya ‘Sangoma’ ikimmtoa mbuzi kafara kwa ajili ya zoezi hilo.
HALI TETE
Ikazidi kudaiwa kuwa, wakati sangoma akisemasema maneno yake ya kufukiza, ghafla alianza kuyumbayumba mpaka kujikuta yupo chini kisha akatulia tuli licha ya wananchi, wakiwemo wanafunzi kumpigia makofi.

WASAIDIZI WAHAHA
Ilibainika baadaye kwamba, sangoma huyo aliyekuwa amelala chali kama kwenye msalaba alikuwa amepoteza fahamu hivyo wasaidizi wake walianza kuhaha kwa kummwagia maji ndoo nzima ili azinduke kama siyo kurejea kwenye uhai wake (pichani).
‘Sangoma’ hao wakimsaidia mmoja wao aliyezidiwa na nguvu za majini.
Sangoma’ wakiendelea kutoa msaada kwa mwenzao aliyeshambuliwa na majini.
CHA AJABU SASA
Cha ajabu sasa, sangoma akiwa hajitambui chini na wasaidizi wake wakiendelea kumzindua, msichana mmoja ambaye hakujulikana jina mara moja, alianza kupagawa, akaishiwa nguvu huku akisemasema maneno yasiyoeleweka, watu ‘waliokula chumvi nyingi’ wakasema amekumbwa na majini.
Mmoja ya raia waliokuwa wakishabikia akiwa hoi baada ya kupigwa na majini.
“Huyo naye ni majini yamemvaa. Huenda yalipokuwa yanatolewa na mganga mengine yakahamia kwake,” alisema mzee mmoja bila kutaja jina lake. Ilibidi wasaidizi wa sangoma huyo wahamie kwake ili kumnusuru na janga hilo ambapo baada ya muda, msichana huyo alirejea katika hali yake ya kawaida.

HALI YATULIA, ZOEZI LASITISHWA
Baada ya sangoma naye kuzinduka, zoezi la kuyatoa majini shuleni hapo lilisimama huku mikakati ikiwekwa kwamba shughuli hiyo itaendelea tena siku kadhaa mbele.
Baadhi ya raia wakishudia yaliyojiri eneo la tukio.
MWENYEKITI WA MTAA ANENA
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kiluvya-Madukani, Adelaida Bruno alisema yeye alipelekewa barua ya maombi kutoka kwa wananchi wake wakimtaka awaruhusu kumuita sangoma kwa ajili ya kuwasaidia kuondoa mambo hayo ya mauzauza shuleni hapo. “Mimi kama serikali, hatuamini ushirikina, niliipokea hiyo barua, nikawaambia kama wamekubaliana kumwita sangoma kuwasaidia basi wafanye wao wenyewe. Na siku hiyo ya sangoma sikuhudhuria,” alisema mwenyekiti huyo.

MWALIMU MKUU ATUPIA KAMATI
Uwazi lilimtafuta mwalimu mkuu wa shule hiyo ambaye hakutaka kujitambulisha jina ambapo alisema siku ya tukio hakuwepo lakini alisikia kutoka kwa watu na kama ni ukweli utakuwepo kwenye kamati ya shule.

No comments: