Thursday, May 17, 2018

DOTNATA APATA PIGO KUBWA!

MASKINI! Mwanamama mkongwe wa filamu za Kibongo, Illuminata Poshi ‘Dotnata’, amepata pigo baada ya kufiwa na mama yake mzazi, Ildegalda Alphonce aliyefariki dunia juzi, Jumatatu, asubuhi katika Hospitali ya Boch, Dar baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Akizungumza na Za Motomoto News, Dotnata alisema kuwa, kifo cha mama yake kimeacha pengo kubwa katika familia kwani kama mzazi, alikuwa na umuhimu mkubwa kwao, lakini ndiyo mapenzi ya Mungu hawawezi kuyapinga.

“Kufiwa na mama siyo jambo dogo, ni kubwa mno, mama yetu ametuachia pengo kubwa na tutamkumbuka sana kwa mengi, ameugua kansa (hakupenda kutaja ya nini) kwa muda mrefu na ameteseka sana kwa kweli ndipo Mungu akaamua kumpumzisha. Tunaumia sana, lakini inabidi tukubaliane na kilichotokea maana kila nafsi lazima itaonja mauti. Tulimpenda mama yetu, lakini Mungu amempenda zaidi,” alisema Dotnata huku akilia kwa uchungu.

Mwili wa mama wa Dotnata ulitarajiwa kusafirishwa kwenda Bukoba mkoani Kagera, lakini mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni walikuwa hawajapanga siku ya kuusafirisha na msiba upo nyumbani kwa dada yake Dotnata, Segerea, Dar. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amen!

No comments: