Wednesday, April 18, 2018

BODI YA MIKOPO (HESLB) YATANGAZA KUANZA KUPOKEA MAOMBI KWA 2018/19


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza kuanza kupokea maombi kwa mwaka wa masomo 2018/19 kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi ujao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na bodi hiyo, mikopo hiyo itaanza kutolewa baada ya kukamilika kwa maboresho ya mfumo wa uombaji mikopo kwa njia ya mtandao.

Katika taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao (www.olas.heslb.go.tz) ambao umefanyiwa maboresho na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM).

Mkurungezi huyo alisema dirisha hilo la maombi ya mikopo litafunguliwa sambamba na kutangazwa kwa mwongozo wa kina utakaotoa utaratibu wa kuwasilisha maombi.

Pia alisema mwongozo huo utatoa utaratibu wa tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi, sifa na vigezo vitakavyotumika katika kuchambua na kutoa mikopo kwa mwaka ujao wa masomo unaotarajiwa kuanza mwezi Oktoba.

"Tunawasihi wale wote wanaotarajia kuomba mkopo wa elimu ya juu kusoma kwa makini mwongozo tutakaoutoa kwa vyombo vya habari na tovuti mwanzoni mwa mwezi Mei, 2018 na kuuzingatia," alisema.

Katika taarifa hiyo, Badru alisema kwa uzoefu wa miaka iliyopita waombaji wa mikopo waliwasilisha maombi yao bila kuzingatia mwongozo uliotolewa na kusababisha baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo.

"Mwaka jana, kwa mfano, zaidi ya waombaji 10,027 kati ya waombaji zaidi ya 61,000 hawakuambatisha nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa au hata vile vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kama tulivyoelekeza," alisema.

Alitaja nyaraka nyingine muhimu ambazo waombaji mikopo wanapaswa kuziandaa ni pamoja na nakala za vyeti vya kitaaluma za kidato cha nne, sita na stashahada ambazo zimethibitishwa na Kamishna wa Viapo - yaani wakili au hakimu.

Aidha, Badru alisema wanafunzi waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu huo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Kituo cha Afya cha Serikali.

Pia alisema wanafunzi ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya sekondari au stashahada (diploma) wawe na barua za uthibitisho wa udhamini huo kutoka katika taasisi zilizogharamia masomo yao.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa HELSB alisema mwaka huu maofisa wa bodi hiyo watatembelea mikoa mbalimbali ili kukutana na waombaji mikopo ili kuwaelimisha taratibu sahihi za kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao.

Alisema ratiba na maeneo itakapofanyia mikutano hiyo itatangazwa mwanzoni mwa mwezi Mei.

No comments: