Thursday, March 1, 2018

WASTARA AREJEA KUTOKA INDIA KWA MATIBABU, YUKO FITI - VIDEO

MSANII wa Bongo Movie, Wastara Juma amerejea Tanzania leo Alhamisi, Machi 1, 2018 akitokea India alikokuwa akitibiwa mguu na mgongo katika Hospitali ya Saifee, Mumbai.

Akifanya mahojiano LIVE na Global TV Online, Wastara amesema kwa sasa yuko ‘fiti’ baada ya kupata matibabu hospitalini na anaweza kusimama mwenyewe na kutembea tofauti kipindi cha nyuma ambapo ilikuwa lazima atumie baiskeli ya walemavu (wheel chair).

“Nilivyofika nilipokelewa kama wagonjwa wengine, nikapata vipimo vya awali na kupewa kitanda, baadaye walikuja madaktari kwa nyakati tofauti ambao walinipima mguu, tumbo na mwingine mgongo. Walibaini maambukizi kwa ndani hivyo nilifanyiwa upasuaji kuuondoa.

“Madaktari waligundua nilikuwa na tatizo la kupungukiwa damu, uvimbe kwenye mguu uliokuwa umekatwa, pia niligundulika kuwa na uvimbe kwenye utumbo na sikuwa najua ambapo nilifanyiwa upasuaji. Hivyo vyote nilifanyiwa upasuaji na kupatiwa dawa.

“Mbali na hivyo nilibainika kuwa na mpasuko kwenye fuvu ‘fracture’ ambayo nimeambiwa nitarudi tena kutibiwa kwani inaweza kuniletea matatizo baadaye. Kwa sasa namshukuru Mungu licha ya kushonwa upya na kupewa mguu mpya, ninaendelea vizuri, mguu ninaufanyia mazoezi. Lakini kwa mgongo maumivu yanazidi kupungua polepole wakati nikifanya mazoezi,” alisema Wastara.

Aidha, Wastara amemshukuru tena Rais John Magufuli kwa kujitoa kwake kumsaidia kufanikisha matibabu yake;

“Namshukuru Rais Magufuli kwa kujitoa kwake, ndoto yangu ilikuwa siku moja nisimame niweze kufanya kazi zangu, na leo hii imewezekana. Kusimama kwangu kunawafanya watu wengi walioko nyuma yangu wanaonitegemea kufanikisha maisha yangu. Uzima huu nilikuwa nauhitaji kwa ajili ya kufanya kazi na hivi karibuni nitasimama,” alisema akielezea shukurani zake kwa Rais.

Wastara aliondoka nchini kwenda India kutibiwa, Jumapili ya Februari 4, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kuchangiwa fedha na watu mbalimbali akiwemo Rais Magufuli.


No comments: