Thursday, March 15, 2018

SERIKALI YALIVALIA NJUGA TATIZO LA NGUVU ZA KIUME

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo, jamii, jinsia na Watoto, Dk Faustine Ndugulile amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya akishirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kufanya utafiti wa afya ya uzazi kwa wanaume ili kubaini sababu za tatizo hilo na kujua ongezeko la upungufu wa nguvu za kiume ni kubwa kiasi gani nchini.

Ndugulile amefikia uamuzi huo kwani mara zote Serikali imekuwa ikitilia mkazo afya ya uzazi kwa mwanamke na kusahau upande wa pili.

Amesema kwa upande wa Tanzania mpaka sasa hakuna tafiti zozote zilizofanyika juu ya tatizo hilo kwa wanaume, hivyo ni wakati wake sasa kulifanyia uchunguzi wa kina na kubaini suluhusho lake.

Aidha kwa tafiti zilizofanywa kisayansi duniani zimebaininsha kuwa wanaume wengi wana matatizo ya nguvu za kiume sababu kubwa ikiwa ni mtindo wa maisha, kwani wengi wao hupendelea kula vyakula ambavyo si bora, vyenye mafuta na sukari kwa wingi ambavyo kwa kiasi kikubwa huchangia magonjwa yasiyoambukizwa na ukosefu wa nguvu za kiume.

Pia tafiti hizo zimeonesha kwamba matumizi ya vilevi ikiwemo pombe na sigara, kutofanya mazoezi mara kwa mara, unene kupita kiasi, msongo wa mawazo, matumizi ya dawa kwa muda mrefu, magonjwa sugu kama kisukari na presha kwa kiasi kikubwa huchangia tatizo hilo.

Katika harakati za kupambana na tatizo hilo Serikali jana imepitisha baadhi ya dawa za tiba asili kutibu tatizo hilo ambazo zimethibitishwa na Mkemia Mkuu na kuruhusiwa kutumika kukabiliana na tatizo hilo dawa hiyo ni Ujana, huku dawa nyingine ambazo zimesajiliwa na zinafaa kutumiwa ni Sildenafil na Tadalafil.

Dawa hizo zimechunguzwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na kuthibitishwa kuwa hazina sumu wala madhara kwa watumiaji na zinapatikana katika maduka mbalimbali ya dawa.

No comments: