Thursday, March 1, 2018

MMOJA AUAWA NA WENGINE WAJERUHIWA BAADA YA MAJAMBAZI KUVAMIA MACHIMBO


WATU watatu  wanaosadikiwa  kuwa ni majambazi wamevamia machimbo ya madini ya   dhahabu  ya Ifumile  Kijiji  cha  Isumamilomo   Wilaya ya  Mpanda na kumuua mchimbaji   mmoja kwa  kumpiga   risasi.

Watu hao wanadaiwa kumpiga risasi ya tumboni  kwa  kutumia  bunduki aina ya AK 47 na kujeruhi wengine watatu.

Pia watu hao wanadaiwa kupora  dhahabu yenye uzito wa zaidi ya gramu 650, fedha  taslimu Sh. milioni 1.5 na   mashine  mbili za kutafutia  dhahabu.

Kamanda  wa  Polisi wa  Mkoa  wa  Katavi,  Damas  Nyanda,  alisema jana alipokuwa anaongea na wandishi tukio  hilo lilitokea  juzi   usiku.

 Alisema  siku   ya  tukio  majambazi hao  ambao  waliokuwa  watatu   walifika  katika machimbo ya  Ifumile  wakiwa  wamejifunika  sura  zao  kininja na  kuwashambulia  kwa risasi wachimbaji na  wanunuzi wa  dhahabu.

Alisema waliwajeruhi wachimbaji watatu  sehemu mbalimbali za miili yao   huku   baadhi wakinusurika  baada  ya kukimbilia kwenye  vichaka.

Kamanda  Nyanda  alimtaja aliyeuawa ni Sita   Kalyalya (34),  mkazi  wa   Bariadi,  Shinyanga   ambae  alipigwa  risasi ya  tumboni   na  mkononi  na alifariki dunia   muda  mfupi  baada ya  kufikishwa katika  Hospitali ya  Manispaa ya   Mpanda  akiendelea   kupatiwa  matibabu.

Aliwataja waliojeruhiwa  ni   Joseph   Panya (34)  ambaye amejeruhiwa kwenye bega  la  kushoto  na  mguu wa kulia,  Mrisho   Rashid (21 )  aliyejeruhiwa   mguuni  na mkono   wa kulia na Masunju  Mgulu  (28)  aliyejeruhiwa     mguu na  mkono wa  kushoto.

Kamanda   Nyanda  alisema  majambazi hao  baada ya  kuwajeruhi  wachimbaji walipora  fedha   hizo, dhahabu na mashine za kutafutia dhahabu kisha kutokomea.

Kwa mujibu wa kamanda huyo,  baada ya tukio  hilo  polisi  walifika  eneo  la tukio na kuokota  risasi  24  na   maganda saba  ya  risasi zilizotumika   za   bunduki iliyotumika  kwenye  tukio  hilo.  Nyanda, alisema   Jeshi la  Polisi linaendelea  kuwasaka  majambazi hao na alitoa  wito  kwa  wananchi  kutoa  ushirikiano kwa  jeshi  hilo  kwa kutoa   taarifa zitakazowawezesha  kuwatia  nguvuni.

Kaimu   Mganga  Mkuu  wa  Hospitali ya  Manispaa ya  Mpanda,  Dk.  Jaffari Masanja,  alisema  marehemu Kalyalya  alifariki muda  mfupi  baada  ya  kutolewa kwenye chumba  cha upasuaji.

Alisema  majeruhi  Panya   na   Rashid walikuwa  wamelazwa  katika  wodi  namba  moja wamepewa  rufaa na  wamesafirishwa  kwenda  katika  Hospitali ya  Taifa ya  Muhimbili  kwa  ajili ya  matibabu  zaidi  baada  ya hali zao kuwa  mbaya,   Alisema Mgulu  amebaki    hospitali  huku  hali hiyo yake  ikiendelea  kuimarika.

No comments: