Friday, September 8, 2017

ZITTO AELEZA USIKU ULIVYOKUWA MGUMU KWAKE



Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.
Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini.
DAR ES SALAAM.  Usiku wa kuamkia leo ulikuwa mgumu zaidi kwenye maisha yangu ya kisiasa, anaeleza Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

"Nimetumia muda mwingi nikitafakari na kumfikiria sana mwanasiasa mwenzangu, kaka yangu, Mbunge mwenzangu na rafiki yangu Tundu Lissu," anasema Zitto katika taarifa aliyoitoa leo Ijumaa.

Lissu alijeruhiwa kwa risasi jana Alhamisi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu katika hospitali ya Aga Khan mjini Nairobi, Kenya.

Mbunge wa Singida Mashariki, Lissu alisafirishwa jana usiku baada ya kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Zitto amesema, "Siku zote, katika maisha yetu ya kisiasa, hata katika mambo tunayotofautiana na kupingana nimekuwa nikiamini kwa dhati kwamba tofauti hizo haziwezi zikatufanya tukashindwa kuvuka salama kama nchi, kama taifa."

Amesema kilichotokea kwa Lissu jana Alhamisi ni kitendo cha kihalifu na kisichoendana na utamaduni wa ustahimilivu wa udugu ambao nchi imekuwa ikisimamia.

"Kitendo kile cha kikatili kinakwenda kinyume kabisa na misingi ya utaifa wetu ambao tumekuwa tukiujenga kwa miaka 25 sasa kwa kuwa na taifa huru kidemokrasia," amesema.

Amesema watanzania wanaolitakia mema taifa wana kila sababu ya kulaani na kukataa utamaduni wa kimafia kuzoeleka nchini.

"Tusimame kulaani kwani huu si utanzania," amehitimisha Zitto katika taarifa yake.

Chanzo: Mwananchi

No comments: