Thursday, September 21, 2017

MAHAKAMA IMEWAACHIA HURU VIGOGO WA MRADI WA MABASI YA MWENDOKASI

pic+vigogo

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo September 20, 2017 imewaachia huru vigogo watatu wa Mradi wa Mabasi ya Mwendokasi (Dart), akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Asteria Mlambo, ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu walipofikishwa Mahakamani wakikabiliwa na kesi  ya kuisababishia Serikali hasara ya Tsh. Milioni 83.5.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 10 wa upande wa mashtaka, vielelezo na ushahidi wa upande wa utetezi ameona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili vigogo hao pasipo kuacha shaka.

Mbali na Asteria Mlambo wengine walioachiwa huru ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Evodius Katale, Mwanasheria Mkuu wa Mradi huo, Francis Kugesha na Mkurugenzi wa kampuni ya Yukan, Yuda Mwakatobe ambapo walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza February 25, 2016.

Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kusababisha hasara ya Tsh Milioni 83.5.

Inadaiwa katika kesi hiyo kuwa September 1 na October 1, 2013 maeneo ya Kinondoni Dar es Salaam, Asteria, Katale na Kugesha wakiwa wafanyakazi wa mradi huo, walishindwa kutekeleza majukumu yao vizuri na kuisababishia Serikali hasara ya Tsh Milioni 83.5.

Katika mashtaka yanayomkabili Mwakatobe, inadaiwa kuwa June 29, 2005 katika ofisi za Kodi Ilala, Dar es Salaam, alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa TRA, wakati akiwasilisha taarifa ya fedha ya mwaka 2004 na 2005 ya kampuni yake ya Yukan Business, jambo lililosababisha alipe kodi ndogo.

No comments: