Friday, May 22, 2015

STEVE NYERERE AJIBU SHUTUMA YA KULA HELA ZA KUJENGEA KABURI LA MAREHEMU ADAM KUAMBIANA

Msanii Steven Mengere a.k.a. Steve Nyerere.

PhotoGrid_1432293123090
Baadhi ya magazeti yaliyoandika kuhusu shutuma hizo.

Na Ipyana Mwaipaja

Kufuatia magazeti pendwa kadhaa kumuandika staa wa bongo movie, Steven Mengere "Steve Nyerere" kuwa amekula hela za kujengea kaburi la marehemu Adam Kuambiana, Steve amejitokeza leo na kukanusha shutuma hizo.
Akizungumza kupitia redio ya Clouds katika kipindi cha Leo Tena, Steve ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bongo Movie,  amekanusha kuwa shutuma hizo si za kweli na kwamba zina lengo la kumchafua tu.

Akielezea kusikitishwa kwake na shutuma hizo, Steve pia ameapa kutojihusisha na masuala ya matatizo ya wasanii tena kutokana na kuchoshwa na kuzushiwa tuhuma za uongo kila mara kuhusiana na masuala ya fedha.

"Kwa kweli nimechoshwa na kila siku watu kunigeuza jalala, kunizushia maneno ya uongo na  kuanzia leo sitaki msanii yoyote anihusishe na masuala kama haya. " amesema Steve.

Katika kipindi hicho, Steve amepambanishwa na msanii Kulwa Kikumba (Dude) ambaye kupitia mtandao wa jamii wa Instagram wawili hao walirushiana maneno ya kulaumiana kuhusiana na  kuzuka kwa kashfa hiyo.  
 
Katika mjadala huo Dude amethibitisha kwamba hakumtuhumu Steve na kwamba yeye hakuandika lolote baya katika mtandao wowote wa kijamii kuhusiana na Steve na sakata hilo.

Hata hivyo, Steve amesema kuwa alitumia ubinadamu kuomba michango ili na wao kama wasanii wawe wameshiriki katika ujenzi wa kaburi hilo na siyo kumuachia mke wa marehemu pekee na kwamba hela hizo hazikupitia mikononi mwake bali zilishikwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Danny Nyalusi ambaye ndiye aliyemkabidhi mke wa marehemu pesa hizo. 

"Kwa jitihada zangu nilifanikiwa kupata pesa taslimu Sh. milioni moja ambazo Sh. laki tatu zilitoka kwa msanii Jacob Stevens (JB) na laki saba kutoka kwa mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na pesa zote ziliwasilishwa kwa mhusika ambaye ni mke wa marehemu" amesema Steve.

Baada ya wawili hao kuwekwa sawa na waendesha kipindi Husna Abdul, Mussa Hussein na Geah Habib, hatimaye wote wawili walikubaliana kuwa yameisha na kuishia kuwalaumu waandishi wa habari kwa kuandika habari bila kuhakikisha wanapata ukweli wa suala zima kutoka kwa wahusika.

No comments: