Saturday, August 17, 2013

TRAFIKI FEKI AJITETEA KUWA UGUMU WA MAISHA NDIO CHANZO



MKANDA mzima wa askari bandia wa Kikosi cha Usalama Barabarani (trafiki), James Juma Hussein (45)  aliyekamatwa saa 1:30 asubuhi ya Agosti, 14, 2013 maeneo ya Tabata Kinyerezi Mnara wa Voda, jijini Dar es Salaam akiwa ndani ya sare zake za kazi, umepatikana....

Kwa nini James alikamatwa? Asubuhi hiyo, afisa mmoja wa trafiki mwenye cheo cha ukaguzi alikuwa akipita eneo hilo kwenda kazini. Alipomwona James alisimamisha gari, akashuka kwenda kumsalimia. Lakini alishangaa kuviona vifungo vya shati lake ni vya kawaida (vya polisi vinatakiwa kuandikwa police force yaani ‘jeshi la polisi’), akamtilia shaka.

Afisa huyo Alimkamata ‘askari feki’ huyo  mkazi wa Kimara Matangini, Dar na kumfikisha kwenye Kituo cha Polisi Stakishari, wilayani Ilala, Dar akafunguliwa jalada namba STK/RB/15305/2013 KUJIFANYA ASKARI ili taratibu za kisheria zichukuliwe juu yake.

Ndani ya kituo cha polisi, James alihojiwa haya:
Askari: Wewe mtu wa wapi?
James: Mnyamwezi wa Tabora.
Askari: Una muda gani ukijifanya trafiki?
 James: Wiki moja sasa.
Askari: Hii kofia ya polisi uliipata wapi?
James: Nguo nyeupe juu ya kofia niliitengeneza kienyeji, krauni, tepe za usajenti na mkanda ni za shemeji yangu alikuwa polisi Tabora, ni marehemu, alikuwa akiitwa Shaban.

James aliwaambia polisi kuwa suruali nyeupe ya kitrafiki aliishona mtaani lakini kamba ya filimbi na kizibao cha kung’ara vilikuwa vya polisi.

Askari: Uliwahi kuwa polisi?
James: Niliwahi kupata mafunzo ya upolisi katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP) mwaka 1990-91 lakini nilifukuzwa kazi kwa sababu nilikwenda muziki. Nilirudi Tabora nikawa mkulima na mke wangu na mtoto mmoja ambao wote sasa ni marehemu.

Ndani ya nguo za kitrafiki alizokuwa amevaa James, alikutwa na suruali ya bluu na fulana ya kijani.

James alisema njaa ndiyo iliyomfanya ajifanye trafiki na ‘kuwapiga mikono’ madereva, hasa wa daladala ili anapowakuta na makosa kwenye magari yao ajipatie chochote.

Kamishina wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Suleiman Kova amethibitisha kukamatwa kwa polisi huyo feki

FILAMU YA "FOOLISH AGE" YA LULU KUZINDULIWA 30 AGOSTI NDANI YA MLIMANI CITY


MSANII mwenye kipaji cha hali ya juu nchini na mwenye umri mdogo, Elizabeth Michael "LULU" anatarajia kuzindua filamu yake ya kwanza toka alipotoka gerezani, iitwayo "Foolish Age".

Filamu hii imetengenezwa na kampuni ya Proin Promotions Limited na itazinduliwa mnamo tarehe 30 Agosti 2013 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Filamu hiyo inayoelezea maisha ya Lulu ni moja ya filamu nzuri na yenye ubora wa hali ya juu kutokana na kutengenezwa na kampuni ya mahiri ya Proin Promotions Limited.

Katika uzinduzi huo, wasanii mbalimbali wakiwemo mwanamuziki Lady Jaydee na bendi yake ya Machozi anatarajiwa kushusha bonge la burudani siku hiyo.

Kupitia mtandao wa kijamii, Lulu aliandika "Nina kila sababu ya kumshukuru Mungu....!! nina furaha ya kuwafahamisha kuwa tarehe  30/08/2013 ndio siku nitakayozindua movie yangu mpya iitwayo FOOLISH AGE..... Hatimaye narudi kazini!!! Uzinduzi utafanyika katika ukumbi wa MLIMANI CITY..... kutakuwepo na wasanii mbalimbali wa muziki..... na pia LADY JAYDEE pamoja na MACHOZI BAND atakuwepo pia!!! nahitaji support ya mashabiki wote wa LULU na mashabiki wa BONGO MOVIE.....*PROINPROMOTERS"

Baada ya uzinduzi wa Filamu hii nakala zitaendelea kuuzwa katika maduka yote ya filamu nchini.  Filamu hii imetengenezwa na itasambazwa na kampuni ya Proin Promotions Limited.

Usikose uzinduzi huu utakaofanyika ndani ya ukumbi wa Mlimani City tarehe 30 Agosti 2013.