ARUSHA: Mrembo
aliyejulikana kwa jina la Doreen Aloyce, anadaiwa kutoweka na michango
ya harusi, hali iliyosababisha wachangiaji kucharuka.
Chanzo makini kililiambia Ijumaa Wikienda kuwa mwanadada huyo
alichangisha michango kwa watu mbalimbali kwa ajili ya harusi yake,
lakini baada ya kupatiwa haikujulikana harusi iliyeyukia wapi.
Wakizungumza baadhi ya wachangiaji hao walimlalamikia Doreen kuwa
wanaona tu picha za harusi huku wakiwa hawajaalikwa siku ya tukio wakati
walichangia pesa zao. “Yaani kwa jumla sisi watoa michango tunashangaa
tumechangishwa michango na kwa kuwa sisi ni shoga yetu na alituomba
tumchangie michango kwa ajili ya ndoa na kwa kuwa ni jambo la heri
tukachanga, lakini siku zilivyozidi kwenda tukaona kimya.
“Kilichotushtua na kutushangaza zaidi ni baada ya kuona anatuma tu
picha za harusi kwenye ukurasa wake wa Instagram akionesha picha kwamba
ameshafunga ndoa. “Kutokana na hilo ikabidi tuanze kuulizana kama kuna
mtu kati yetu ambaye amehudhuria, lakini kila mmoja alikataa, tukabaki
tunajiuliza kwa nini ametufanyia hivi?“Michango ametuchangisha na picha
zenyewe bwana harusi sura yake haionekani, kitu ambacho kimetutia shaka
pia kuwa hii ndoa huenda amechukua michango yetu na kupiga picha tu
akiwa amevaa shela ili tuone kuwa ameshafunga ndoa.
“Tunachotaka sisi ni michango yetu airudishe na siyo vinginevyo,”
alisema mmoja wa wachangiaji wa harusi hiyo kwenye kundi la WhatsApp.
Ili kuujua ukweli wa madai hayo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta bi harusi
huyo ambaye alisema yupo Zanzibar kwenye mapumziko baada ya kufunga
ndoa.
Alieleza kuwa kuna sababu iliyomfanya kufunga ndoa hiyo, lakini
alipotakiwa kutaja jina la mumewe alikataa. “Ni kweli nilifanya
michakato ya harusi yangu, kwa hiyo nilifanya harakaharaka kwa kuwa mume
wangu alikuwa nchini Sweden, niliwachangisha watu kweli, lakini
ulitokea msiba kwenye familia yangu na ikabidi tusogeze mbele kila kitu
wanajua.
“Kwa hiyo mume wangu alikuja huku ikabidi tufunge ndoa harakaharaka
kwa sababu ya msiba.“Wachangiaji walianza kunipigia simu na kusema mbona
situmi picha na wao walitaka waje wale na kunywa, kwa nini nimefungia
ndoa mbali yaani Zanzibar, lakini niliwapa taarifa kuhusu kusogeza mbele
tarehe ya harusi.
“Sasa wakaanza kusema kwamba mimi nimeposti picha, lakini sura ya
mume wangu nimeificha. “Ni kweli nilificha sura ya mume wangu kwa sababu
kwa mila zetu na pia najua mimi ni mwandishi wa habari nilishaelekezwa
na wakongwe wa tasnia ya uandishi kuwa nisimuanike mume wangu kwa kuwa
itakuja kuwa shida waandishi watamfuatafuata mpaka nyumbani.
“Baada ya kupata simu zao wakinilalamikia nilimweleza mume wangu
akaniambia niwaambie waandike majina yao ili tuweze kuwarudishia pesa
zao kwa sababu mtu anapoanzisha jambo kubwa kama hilo, lazima awe
amejiandaa, michango ni ya ziada tu hivyo ninawarudishia michango yao,”
alisema Doreen ni mwandishi wa habari mkoani Arusha.
STORI: NEEMA ADRIAN, Wikienda
No comments:
Post a Comment