Wednesday, March 21, 2018

DKT MWAKYEMBE AKERWA NA KAULI ZA DIAMOND; SASA KULA NAYE SAHANI MOJA

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ameeleza kukerwa kwake na mwanamuziki Diamond Platnumz kutokana na kumdhalilisha Naibu wake, Juliana Shonza wakati akihojiwa katika kipindi cha The Play List cha redio ya Times FM na mitandaoni.

Katika maelezo yake Mwakyembe amesema kuwa inawezekana kwa sasa Diamond ameanza kulewa sifa na umaarufu alio nao mwanamuziki huyo.

Amesema kuwa serikali imekaa vikao vingi na wasanii lakini Diamond hahudhurii kwa hiyo si wajibu wa Serikali kumfanyia kikao chake mwenyewe kutokana na umaarufu wake.

“Hatuwezi kuwa na sheria kwa wasanii wengine na sheria maalum kwake, nadhani hizi ni dalili za kuanza kulewa umaarufu kwani Diamond si Kiongozi wa Shirikisho la Muziki wala msemaji wa Chama cha Muziki wa kizazi kipya kuwasemea wenzake,” amesema Dkt. Mwakyembe.

Hata hivyo, Dkt. Mwakyembe amemshauri mwanamuziki huyo asishindane na Serikali na kama ana ushauri autoe kistaarabu utazingatiwa lakini si kwa kumshambulia Naibu Waziri kwa dharau na kejeli kama jinsi alivyofanya, kitu ambacho amesema hajafurahishwa nacho hata kidogo.

No comments: