Wednesday, March 21, 2018

MBARONI KWA MAUAJI YA MKEWE NA KIFICHA MWILI KWENYE MBUYU MIAKA NANE

Mabaki ya mwili wa marehemu Tabu Robert.
MKULIMA Benard Shumbi (47) mkazi wa Yulansoni wilayani Mkalama mkoa wa Singida, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya mkewe anayedaiwa kumtumbukiza ndani ya pango la mbuyu tangu mwaka 2010, kisha akaripoti polisi kuwa haonekani nyumbani.

Mabaki ya mwanamke huyo, Tabu Robert aliyekuwa na umri wa miaka 28 wakati huo yalipatikana Jumamosi baada ya polisi kumhoji na kukiri kuua, kisha kuwapeleka hadi kwenye pango la mti huo uliopo umbali wa mita 600 kutoka nyumbani kwake.
Zoezi la utoaji mwili wa marehemu Tatu Robert likiendelea.

Wananchi wakishuhudia mti ambao mwili wa marehemu Tabu Robert ulikuwemo kwa miaka 8 bila kugundulika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Dobora Mgiligimba alisema mauaji hayo yanadaiwa kufanywa Septemba 7, 2010, saa mbili usiku nyumbani kwa mtuhumiwa.

Alisema baada ya kumuua mkewe, mtuhumiwa aliubeba mwili hadi kwenye mbuyu na kuutumbukiza ndani, kisha akatoa taarifa polisi kuwa mkewe amepotea.

“Machi 17, mwaka huu (Jumamosi), Polisi tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa Tabu hakupotea bali aliuawa na mumewe," alisema Kamanda Mgiligimba.

 
"Tulipomhoji, alikiri akatupeleka mpaka kwenye huo mbuyu, akatuonesha shimo kubwa ambalo alimtumbukiza mkewe baada ya kumuua.”

Magiligimba alifafanua kuwa polisi walipoingia ndani ya pango hilo waliyakuta mabaki ya mwili wa mwanamke huyo - mifupa mbalimbali na fuvu la kichwa - kisha kuyachukua na hatimaye kuwakabidhi ndugu zake kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Alisema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni ulevi wa pombe za kienyeji wa marehemu, ambapo mtuhumiwa aliona ni kero kuachiwa mtoto mwenye umri wa miaka miwili, Alisema mtuhumiwa aliamua kumpiga mkewe hadi kusababisha mauti yake.

Kamanda Magiligimba alisema polisi inakamilisha uchunguzi wa tukio hilo ili mtuhumiwa aweze kushtakiwa mahakamani kwa kosa la mauaji.

Kutokana na tukio hilo, Magiligimba alisema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi; hasa wanandoa kuacha kujichukulia sheria mkononi ikiwemo kutoa vipigo vikali.

Aidha, kamanda huyo alitaka jamii kutoa taarifa mapema za uvunjifu wa amani ili kuwabaini wahalifu.

No comments: