Friday, November 24, 2017

WATU 10 WAFARIKI KATIKA AJALI


Watu 10 wamefariki na wengine 24 kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Hiace, kugongana uso kwa uso na gari dogo aina ya Toyota Noah katika eneo la Ihuka wilayani Ikungi Mkoani Singida.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Deborah Magiligimba amesema ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa dereva wa gari aina ya Toyota Hiace T581 BBV kulifuata gari aina ya Toyota Noah namba T423 CFF na kusababisha vifo na majeruhi.

Kamanda Magiligimba amesema kuwa gari moja kati ya hayo lilikuwa linatokea kumchukua Bibi Harusi wakati gari nyingine ilikuwa inatokea kwenye msiba ndipo zilipokutana katika eneo hilo na kusababisha ajali ambayo taarifa za awali zinasema imetokana na uzembe wa dereva.

Mganga wa zamu katika Hospitali ya Malkia wa Ulimwengu Puma Singida, John Mmary amethibitisha kupokea miili ya marehemu hao pamoja na majeruhi wa ajali hiyo ambao wengi wao walikuwa katika gari aina ya Toyota Hiace na kuongeza kwamba majeruhi kumi na tano waliolazwa katika hospitali hiyo wanaendelea vizuri na matibabu isipokuwa wawili hali zao siyo nzuri na wameumia sehemu kubwa za vichwa.

Magari yaliyo gongana aina ya Hiace inadaiwa lilikuwa limewabeba maharusi pamoja na ndugu zao huku gari aina ya Noah ilikuwa imewabeba watu waliokuwa wakitokea kwenye msiba.

No comments: