Friday, October 9, 2020

MSHUKIWA WA MAUAJI YA GEORGE FLOYD AACHILIWA KWA DHAMANA

 

Polisi wa zamani wa Marekani Derek Chauvin aliyeachishwa kazi baada ya kushitakiwa kwa mauaji ya mwanaume mweusi ambaye hakuwa amejihami, George Floyd ameachiliwa kutoka jela kwa dhamana ya dola za Marekani milioni moja.

Afisa huyo mzungu alirekodiwa kwenye kanda ya video akipiga goti kwenye shingo ya Floyd kwa karibu dakika nane kabla ya kufariki dunia Mei 25.

Kifo cha Floyd kilisababisha maandamano makubwa nchini Marekani kushinikiza mageuzi katika idara ya polisi, yakiongozwa na vuguvugu la Black Lives Matter.

Chauvin alifutwa kazi na sasa anasubiri hukumu dhidi yake baada ya kushitakiwa kwa mauaji ya kiwango cha pili na kuua bila kukusudia mwezi Machi huku maafisa wengine watatu J Alexander Kueng, Thomas Lane na Tou Thao ambao pia walifutwa kazi na walishitakiwa kwa kutowajibika, tukio la mauaji likifanyika mbele yao.

Maafisa wote wanne wanaotuhumiwa kwa mauaji ya Floyd huko Minneapolis, Minnesota, wamelipa dhamana na wako huru wakisubiri hukumu dhidi yao kutolewa mwakani.

Chauvin alikuwa anashikiliwa katika jela ya Oak Park Heights, Minnesota, tangu mwishoni mwa Mei.

Ben Crump, wakili na mwanaharakati wa kutetea haki anayewakilisha familia ya Floyd, amesema kuachiliwa kwa Chauvin kwa dhamana kunawakumbusha machungu na kwamba bado wako mbali na kupata haki ya Floyd.

“Japo George Floyd alinyimwa haki akiwa hai, hatutarudi nyuma hadi atendewe haki akiwa amekufa,” amesisitiza Crump.

Kwa sasa, maafisa wote wanne wamepangiwa kuhukumiwa pamoja mwezi Machi 2021, lakini jaji inatafakari uwezekano wa kila mmoja wao kuhukumiwa kivyake.

(Chanzo: dar24.c0m) 

No comments: