Wednesday, May 2, 2018

WOSIA WA KIFO CHAKE, WEMA KUZIKWA KIKRISTO?

KUFUATIA wosia wa kifo chake ulioeleza namna anavyotaka mazishi yake yawe siku atakapokufa, staa mkubwa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu ameibua sintofahamu na kusababisha baadhi ya watu kuhoji kuwa anataka azikwe kwa Dini ya Kikristo? Risasi Mchanganyiko linaye.

Katika mahojiano na gazeti ndugu la hili, Ijumaa Wikienda, toleo la Jumatatu iliyopita, Wema alikaririwa akisema kuwa, siku akifa, aagiwe msikitini na si kwingineko.

Katika wosia wake huo, mbali na hilo, Wema aliongeza utata baada ya kusema kuwa kwenye mazishi yake wahudhuriaji wapendeze, wafurahie maisha aliyokuwa akiishi na katika nyumba itakayokuwa na msiba wake, papambwe rangi ya pinki na staa mwenziye, Aunt Ezekiel ndiye awe wa kwanza kuweka maua kwenye kaburi lake.

Baada ya habari hiyo kuingia mitaani na kuwa gumzo, baadhi ya watu walijikita kwenye kuhoji dini ya staa huyo ambapo baadhi yao walimpinga kwamba, katika taratibu za mazishi ya Kiislam hakuna mambo hayo ya rangi ya maua, kuagwa na kuwekewa mashada.
Wema akiwa na rafiki yake Anty Ezekiel (kulia).
“Ninavyojua mimi Wema ni Muislam, sasa sijui hilo ua Aunt ataliweka lini kwa sababu wanawake huwa hawaruhusiwi kwenda makaburini, labda akienda, awe anakwenda kufanya usafi na aingie kwa dua maalum ya kuingia makaburini,” ilisomeka sehemu ya maoni kibao kwenye ukurasa wa Global Publishers wa Facebook yaliyokuwa yakimkosoa Wema juu ya wosia wake.

Kufuatia mjadala huo mzito aliouibua, Risasi Mchanganyiko lilimuuliza Wema juu ya hilo ambapo mambo yalikuwa hivi;

Risasi Mchanganyiko: Umeeleza unavyotaka mazishi yako yawe, lakini mbona mambo unayoyasema huwa hayapo kwenye dini yako ya Kiislam?

Wema: Kwani baba yangu (marehemu Balozi Isaac Abraham Sepetu) alizikwaje?

Risasi Mchanganyiko: Alizikwa Kikristo, lakini wewe watu wanajua ni Muislam! Ina maana utabadili dini?

Wema: Wataamua ndugu zangu. Hayo niliyoyaeleza ni endapo ndugu zangu wataamua nizikwe Kikristo kama baba yangu, lakini kama wataamua nizikwe kwa dini yangu ya sasa hivi (Uislam), basi hayo hayatakuwepo badala yake watafuata matakwa ya dini husika.

No comments: