Thursday, April 5, 2018

ZITTO KUMSINDIKIZA NONDO UHAMIAJI, AWAITA WAZEE WA UJIJI KUMALIZA MAMBO


KIONGOZI WA Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema atamsindikiza Mwenyekiti Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo katika Ofisi za Makao Makuu ya Uhamiaji hapa nchini.

Zitto amesema hayo baada ya taarifa kusambaa kuwa, Nondo amepata wito wa barua akitakiwa kufika uhamiaji ili akahojiwe kuhusu taarifa za uraia wake pamoja na za ndugu zake.

“Siku hiyo Uhamiaji watatuambia kama Kigoma sio Tanzania ili tuwaombe wasio wa Kigoma warudi Tanzania, haiwezekani waliyo wengi pasiwe kwao, wachache ndiyo iwe kwao,” alisema Zitto.

Taarifa hizo zilieleza kwamba, sheria inawaruhusu uhamiaji kumuhoji mtu yeyote wanaotilia mashaka juu ya uraia wake, na kuwa wana mashaka na uraia wa Abdul Nondo, hivyo awathibitishie kuwa yeye ni Raia wa Tanzania.

Taarifa za kupotea kwa Nondo katika mazingira ya kutatanisha ziliibuka Machi 6 mwaka huu baada ya kutuma ujumbe kwa mmoja wa marafiki zake usiku wa manane akisema kuwa usalama wake uko hatarini.

Hali hiyo ilipeleka taharuki miongoni mwa wanafunzi wenzake na jamii kwa ujumla huku wengi wakidhani kuwa Nondo alikuwa ametekwa. Nondo anatakiwa kurudi uhamiaji Aprili 20 na kupeleka cheti chake cha kuzaliwa, cheti cha kuzaliwa cha baba yake, mama yake, cha bibi na babu mzaa baba na mzaa mama.

No comments: