Thursday, April 5, 2018

TABORA: BASI LA CITY BOY LAGONGANA NA FUSO USO KWA USO, 12 WAFARIKI, 46 WAJERUHIWA


BASI la Kampuni ya City Boys limepata ajali ya kugongana na lori aina ya Fuso katika eneo la Makomero Tarafa na Wilaya Igunga Mkoa wa Tabora usiku wa kuamkia leo na kusababisha vifo vya watu 12 na wengine 46 kujeruhiwa.

Kaimu Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Tabora, Inspekta Hardson, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni tairi la kulia la Fuso kutumbukia kwenye mashimo mawili na kusababisha tairi kupasuka na rimu kupinda hivyo likakosa mwelekeo na kuligonga basi la City Boy uso kwa uso.

Inspekta Hardson amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya igunga huku baadhi ya majeruhi wakipelekwa Hospitali ya Nkinga na wengine Bugando Mwanza kwa ajili ya matibabu.


TAARIFA YA AWALI YA AJALI YA CITY BOY NA FUSO KUTOKA TRAFFIC TABORA

Nimefika eneo la tukio saa 5.30 usiku toka Tabora mjini 200Kms. Eneo ni Makomero tarafa na wilaya Igunga mkoa wa Tabora.

Gari T486 ARB aina ya FUSO likiwa na mzigo wa viazi ikitokea Singida kuelekea Igunga tairi ya kulia limetumbukia katika mashimo mawili barabarani kisha kupasua tairi na rim kupinda na mfumo wa usukani kukatika maungio ya steering rod na steering box kisha gari kukosa uelekeo na kugonga basi la abiria T983 DCE Scania kampuni ya City boy.

Jumla ya watu 12 wamepoteza maisha, 10 eneo la tukio, 2 wakiwa wanapelekwa Hospitali ya Wilaya Igunga.

Jumla ya majeruhi 46 wamefikishwa Hospitali ya Wilaya Igunga kwa matibabu, kati yao 3 ni mahututi ambapo wanaume wawili wamepelekwa Bugando Mwanza na mwanamke mmoja amepelekwa Nkinga usiku huu.

Dereva wa basi amefariki papo hapo. Wahusika wa FUSO kwa taarifa za awali inasemekana wamekimbia baada ya ajali hii.

No comments: