Thursday, April 5, 2018

SERIKALI YAAHIDI KUPUNGUZA KODI


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango.

SERIKALI imetangaza neema kwa wenye viwanda wa ndani baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kutangaza kuwapunguzia kodi kadri itakavyowezekana katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Dk. Mpango atasoma hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha wa 2018-2019 siku 70 kuanzia leo.

Dk. Mpango alitangaza neema hiyo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zainab Katimba.  Pia alilithibitishia Bunge kuwa amepokea mapendekezo ya maboresho ya kodi, zikiwemo za mifugo.

Katika swali lake la nyongeza, Katimba alisema mkakati wa kufikia uchumi wa viwanda unalenga kutatua changamoto ya ajira; hususan ya vijana lakini viwanda vya ngozi vinakabiliwa na changamoto kubwa kupata malighafi.

"Je, serikali ina mpango gani wa kutoa punguzo la kodi kwa viwanda vinavyozalisha mazao yanayotokana na mifugo ili kufikia malengo?" Alihoji Mbunge huyo.

Akijibu, Dk. Mpango alisema amepokea mapendekezo ya kodi mbalimbali na anathibitisha kwamba mapendekezo yaliyotoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi yamefika Wizara ya Fedha.

"Hapa mikononi mwangu nina kitita cha kurasa 53 ya mapendekezo ya maboresho ya kodi mbalimbali ikiwemo ya sekta ya mifugo," alisema Dk. Mpango hivyo "mbunge avute subira kidogo serikali itatangaza kupitia hotuba yake kuu ya serikali.

"Lakini nimhakikishie kuwa ni dhamira ya serikali kuhakikisha viwanda vya ndani vinapewa ahueni ya kodi mbalimbali kadri itakavyowezekana."

Awali, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalla Ulega alisema wizara hiyo imepeleka mapendekezo Wizara ya Fedha kuhakikisha kodi zote zinazotozwa katika vifaa vya uchakataji wa ngozi zipunguzwe au kuondolewa kabisa ili kuhamasisha uwekezaji zaidi kwenye sekta ndogo ya ngozi.

"Sambamba na hili tumehakikisha tunapendekeza Wizara ya Fedha iweze kuongeza viwango (vya ushuru) kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi kuingia nchini hasa za mitumba," alisema Ulega.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Katimba alitaka kujua kama serikali haioni ni wakati muafaka wa kupiga marufuku uingizwaji wa nyama kutoka nchi za nje ili kuruhusu ukuaji wa viwanda vya nyama nchini.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ulega alikiri kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika baada ya Ethiopia.

Aidha, alisema kumekuwepo na uingizaji wa nyama ya ng'ombe, nguruwe na kondoo kwa wastani wa tani 2,000 kwa mwaka kuanzia 2013-2015.

Hata hivyo, kiasi hicho kimepungua kuanzia mwaka 2016, alisema ambapo ziliingia tani 1,182.79 na mwaka 2017/18 tani 1,225 kutokana na kuwepo kwa machinjio na viwanda 23 vyenye uwezo wa kuzalisha tani 44,820.6 za nyama na bidhaa zake kwa mwaka; zenye ubora linganifu na nyama inayotoka nje ya nchi.

Alisema kwa mwaka 2016/17 jumla ya nyama tani 2,608.93 yenye thamani ya dola za Kimarekani 5,676,217.28 (Sh. bilioni 12.8) iliuzwa katika masoko ya nje ya Oman, China, Hongkong, Dubai, Vietnam.

"Vilevile, idadi ya machinjio nchini kwasasa ni 1,632 na yana uwezo wa kuchinja nyama kiasi cha tani 625,992 kwa mwaka," alisema zaidi.

"Pia masoko ya nyama inayozalishwa ndani ya nchi yameongezeka ambapo inauzwa katika hoteli za kitalii, maduka maalum na migodi yote nchini."

No comments: