Friday, March 9, 2018

MWILI WA MTANZANIA ALIYEUAWA AFRIKA KUSINI WAWASILI NCHINI, KUZIKWA KASULU LEO

Dar es Salaam. Mwili wa mwanafunzi Mtanzania aliyeuawa Afrika Kusini wiki mbili zilizopita umewasili nchini juzi usiku.

Baraka Nafari aliyekuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Mwanza aliuawa usiku wa kuamkia Februari 23, huko Johannesburg, Afrika Kusini na watu wasiofahamika, Habari zinasema aligongwa na gari mara mbili kwa kubamizwa ukutani.

Nafari alikuwa nchini humo akichukua masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Johannesburg na alitarajiwa kuhitimu Juni mwaka huu.

Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema, mwili wa Mtanzania huyo uliwasili nchini juzi usiku na unatarajiwa kusafirishwa leo saa tatu asubuhi kwenda Kigoma na baadaye Kasulu kwa mazishi; Mke wa marehemu, Naomi Baraka alithibitisha kuwasili kwa mwili huo.

“Tumearifiwa kwamba mwili wa marehemu utawasili Kigoma kesho (leo) saa tano asubuhi na baada ya hapo utasafirishwa hadi Kasulu ambako nadhani kama mambo yatakwenda sawa tutazika alasiri,” alisema Naomi.

Baada ya mwili wa marehemu Nafari kufikishwa jijini Dar es Salaam Jumatano saa mbili usiku ulihifadhiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere hadi leo alfajiri ambako unatarajiwa kusafirishwa kwa ndege ya Air Tanzania kwenda Kigoma.

Binamu wa marehemu, Uwezo Edward, anayeishi Cape Town alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema utata wa mazingira ya mauaji yametokana na ushahidi wa video ya (CCTV) wa siku ya tukio katika eneo alipokuwa ndugu yake huyo.

Alisema video ya CCTV, inaonesha Nafari na mwenzake walikuwa wanafuatiliwa nyuma na teksi ambayo ilikuwa na watu wawili ndani yake.

Uwezo alisema kufuatiliwa kwa tukio hilo na polisi wa Afrika Kusini kulianza baada ya yeye kutoa taarifa katika ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Taarifa ya wanafunzi ilikosoa kile ilichokiita kuachiwa katika mazingira ya utata kwa wahusika wa tukio hilo ambao tayari walikuwa wametiwa mbaroni na polisi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga akizungumza na vyombo vya habari alithibitisha kifo cha mwanafunzi huyo na kwamba walikuwa wakifuatilia taarifa zaidi kupitia ubalozi.

No comments: