Wednesday, March 14, 2018

BREAKING NEWS: TAKUKURU WA YAMKAMATA AFISA KINONDONI (VIDEO)

Na Ipyana A. Mwaipaja
Afisa Usafi na Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Alban Gerald Mgebuso anatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa kwa tuhuma za  kupatikana na kosa la kudai na kupokea rushwa.

Akisoma taarifa kwa umma leo asubuhi mbele ya waandishi wa  habari, Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kinondoni, Eugenius Bernard Hazinamwisho amesema afisa huyo aliwekewa mtego siku ya tarehe 3 Machi mwaka huu na kufanikiwa kutiwa nguvuni.

Afisa huyo anatuhumiwa kupokea rushwa ya shilingi milioni moja ili aweze kuliachia gari lililokuwa na kosa la kuchota mchanga bila kibali.

"Mgebuso aliomba rushwa ya shilingi milioni 1.5 na kupokea milioni 1 ili aliachie gari alilokuwa amelishikilia na kulipaki katika yadi ya Manispaa, Mwananyamala kwa madai ya dereva wa gari hilo kuchota mchanga kutoka katika mto Nyakasangwe uliopo kata ya Wazo." amesema Hazinamwisho.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa dereva huyo aliambiwa kosa lake lilitakiwa alipe faini ya shilingi milioni 3 ila mtuhumiwa aliomba apewe milioni 1.5 ili amfutie kosa hilo.

Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa, lililoainishwa katika kifungu namba 15/1A cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa.


No comments: