Tuesday, December 12, 2017

UKATILI WA KIJINSIA WAMUINGIZA TRUMP MATATANI


Wanawake watatu wamemtuhumu Rais Donald Trump kwamba aliwafanyia ukatili wa kijinsia miaka iliyopita kabla hajawa Rais na hivyo Baraza la Congress linamchunguza Trump kutokana na kashfa hizo.

Wanawake walioibua kashfa hiyo dhidi ya Rais Trump ni Jessica Leeds, Samantha Holvey na Rachel Crooks ambao wamesema kuwa Rais Trump bila ridhaa yao alikuwa akiwashikashika, kuwabusu kwa nguvu na ukatili mwingine. Lakini hata hivyo ikulu ya White house imesema kuwa madai ya wanawake hao si ya kweli.

"Rais alikwisha elezea wazi wazi kashfa hizi katika mikutano yake ya kampeni hata kabla hajawa Rais na tunaamini kuwa madai haya yalikwishajibiwa kwa mfumo huo." Sarah Huckabee Sanders.

Rachel Crooks katika madai yake dhidi ya kashfa hiyo ya Rais Trump anasema kuwa yeye alilazimishwa kupigwa busu na Rais Trump nje ya lift ya majengo ya ghorofa za Trump enzi hizo akiwa na miaka 22. Japokuwa mkasa huo ulitokea miaka mingi iliyopita, anasema bado Trump anapaswa kuchukuliwa hatua.

Mwanamke mwingine anayemtuhumu Rais Trump ni mlimbwende wa mwaka 2006 Bi Samantha Holvey ambaye anasema, Trump alihudhuria mashindano hayo na alikuwa anawakagua mwilini kama vile nyama inavyokaguliwa buchani, na amesema kuwa hana nia ya kumchukulia hatua Rais Trump bali anaweka wazi kile alichofanyiwa.

Rais Trump tangu aingie madarakani amekuwa akiandamwa na kashfa mbali mbali zikiwemo za kisiasa na zile zinahusiswa na biashara zake.

No comments: