Friday, December 2, 2022

MABASI YOTE YA SHULE KUWA NA MAKONDAKTA WA KIKE - DKT. GWAJIMA

 

Serikali imeagiza mabasi yote yanayobeba wanafunzi kuwa na kondakta wa kike na mabasi yote yafungwe kamera maalum.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ametoa agizo hilo alipokuwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe katika Shule ya Star LightPre and Primary School, ambapo mtoto wa miaka sita wa darasa la kwanza anadaiwa kubakwa na kondakta wa gari hilo.

Dkt. Gwajima amesema "watuhumiwa kwa sasa  wapo ndani na wameshapanda mahakamani, pongezi wote waliowajibika haraka kesi inaendelea," amesema Gwajima.

Aidha Dkt. Gwajima amesema ana uhakika kuwa suala hilo halitaleta shida kwa kuwa hakuna gharama yoyote itakayoongezeka kwa kuwa ni jinsia tu ndio inabadilika.  Hii itawezesha ulinzi imara kwa mtoto wa kwanza kuchukuliwa na wa mwisho kurejeshwa,”             

"Tunaangalia uwezekano huko mbele kuwe na haja ya kufunga kamera kwenye mabasi ya shule. Lazima wateja walindwe yaani mtoto ni mteja jamani inakuwaje analipia huduma alafu anafanyiwa vitendo vya kikatili?" aliongeza Waziri Gwajima.

Tamko hilo la Serikali linakuja ikiwa ni siku chache baada ya kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii inayoelezea mtoto wa miaka sita kubakwa na dereva na kondakta wa basi la shule.

Source: Habari Leo instagram

No comments: