Wednesday, May 9, 2018

SERIKALI YAITAKA MENEJIMENTI YA TAZARA KUPUNGUZA IDADI YA WATU

SERIKALI imeitaka Menejementi ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kupunguza idadi ya ukubwa wa menejimenti ili kubaki na watu wachache wenye uwezo wa kuzalisha na kufanya kazi kwa weledi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua mfumo maalum wa kieletroniki kwa ajili ya kufuatilia mizigo ya wateja kujua ulipo wakati inasafirishwa na kusaidia kuondoa upotevu.

Alisema licha ya kwamba Tazara imeanza kuboresha miundombinu, kumekuwa na changamoto katika taasisi hiyo ikiwamo suala la uongozi.

Mbarawa alisema ni jambo la kushangaza kuwapo kwa viongozi katika shirika kwa miaka 10 ambao hawana mchango katika uzalishaji, hivyo inabidi menejimenti  kupunguza idara kutoka 15 hadi nane au sita na kuwa na wakurugenzi ambao  watafanya kazi kwa ufanisi.

“Tazara mfanye linalowezekana kupunguza matumizi yasiyo ya msingi. Lengo la serikali ni kuhakikisha mashirika yanajiendesha ili yajitegemee badala ya kuitegemea serikali,” alisema Mbarawa.

Aidha, Waziri Mbarawa alizindua mabehewa 10 na vichwa viwili vya treni ambayo alisema yalikuwa mabovu kwa miaka 10 baada ya kupata ajali na sasa Tazara imeyafufua na yanaweza kufanya kazi kwa miaka mingine zaidi ya 15.

Alisema mabehewa hayo ni kwa ajili ya kubebea kokoto na yametengenezwa na wazawa katika karakana ya Tazara iliyoko mkoani Mbeya kwa gharama ya Sh milioni 167 na kwamba yangenunuliwa mapya serikali ingelipia Sh. bilioni 17.

Mbarawa alisema kwa sasa vichwa 10 vya treni ndivyo vinavyofanya kazi kukiwa na mabehewa ya mzigo na ya abiria na kuishawishi Tazara kuona umuhimu wa kununua vichwa vipya angalau kila mwaka kimoja au viwili.

Akizungumzia mfumo aliozindua, Waziri amewataka watendaji wakuu waujue ili yasije yakatokea yale ya Shirika la Posta kwa kuwa mtendaji wake alishindwa kufungua mfumo na kwamba hali hiyo inaweza kusababisha hujuma kama mhusika hajui kazi inavyofanyika.

Naye Meneja Mkuu wa Tazara Mkoa wa Dar es Salaam, Fuad Abdallah,  alisema mfumo uliozinduliwa una manufaa kwa Shirika hilo kwa kuwa unaboresha suala zima la usimamizi wa treni.

Alisema ni mfumo wa kwanza katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata kwa nchi za Afrika ya kati na umetengenezwa na wazawa na mteja hana haja ya kupiga simu katika kitengo kinachosimamia treni kwa ajili ya kuulizia mizigo  kuwa anaweza kuona kupitia simu yake ya mkononi.

No comments: