Tuesday, May 8, 2018

INAUMA SANA, MTOTO AMWAGIWA MAFUTA YA MOTO!

INAUMA sana! Mtoto Minza Jonas (4), mkazi wa Kitongoji cha Madarasa jijini Mwanza amepita kwenye bonde la mauti na maumivu makali baada ya kumwagia mafuta ya kula yakiwa ya moto.

Akisimulia mkasa huo wa kutisha na kusikitisha, mama Minza, Ester Lucas alisema kuwa, bintiye huyo alifanyiwa ukatili huo uliopitiliza na mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa) ambaye baada ya kutenda unyama huo alikimbilia kusikojulikana.

Ester alisema kuwa, siku ya tukio la kuunguzwa mwanaye huyo ambalo lilijiri miezi mitatu iliyopita, yeye alikuwa ndani kwake ndipo akasikia mtoto akimuita na kumwambia kuwa Minza alikuwa ameunguzwa kwa kumwagiwa mafuta ya kukaangia maandazi.

Alisimulia: “Yaani nilitoka ndani kwa kasi sana, nikaenda kumuona mwanangu. Nilimkuta ameshaanza kuvimba mwili huku akiwa ameshikwa mkono na mtoto mwenziye.

“Cha ajabu, karai alilokuwa akikaangia maandazi yule mama lilikuwa lipo chini, lakini yeye hakuwepo.”

Aliendelea kusimulia kwamba, alijaribu kumuita huyo mama ambaye ndiye alikuwa akikaanga maandazi, lakini hakumjali badala yake alichukua maji na kwenda bafuni kuoga. Mama Minza alisema kuwa, kitendo hicho kilimuumiza hivyo ilibidi amchukue mtoto wake na kumkimbiza Hospitali ya Sekou Toure jijini Mwanza.

Mama huyo aliendelea kusema kuwa, kwa kuwa alikuwa amechangayikiwa, hakuweza hata kumpa taarifa baba mtoto wake huyo na badala yake alipitiliza moja kwa moja hadi hospitalini. Alisema kuwa, baada ya muda, mumewe alipewa taarifa ambapo alifika hospitalini hapo.

“Mume wangu alipofika nilimweleza kisa kizima cha mwanetu kumwagiwa mafuta ya moto na jinsi nilivyomkuta akiwa ameumuka.

“Nilimweleza gharama ambazo zilitakiwa kulipwa pale hospitalini ili mtoto apate matatibu, lakini alisema gharama ni kubwa hivyo aliniambia ngoja akatafute hizo pesa na hakurudi tena,” alisema Ester au mama Minza.

Mama Minza aliendelea kusimulia kuwa, cha kushangaza zaidi, mwanamke aliyetuhumiwa, hakuwahi kufika hospitalini hata mara moja badala yake, baada ya tukio hilo alihama na hakuonekana tena.

“Nilichanganyikiwa sana, hata polisi sikukumbuka maana nilitaka tu mtoto wangu apate uhai kwani aliungua vibaya sana na mpaka sasa anahitaji kufanyiwa upasuaji.

“Kingine kinachonipasua kichwa ni kwamba mdomo wake hauwezi kufunga vizuri kama awali hivyo lazima uwekwe sawa,” alisema mama huyo na kuongeza kwamba anaomba msaada wa hali na mali.

Kama umeguswa na habari hii na unahitaji kumsaidia mama Minza, unaweza kuwasiliana naye kwa namba yake ya mkononi ya 0744 894 649. 
Shukrani zimwendee Mtangazaji wa Kipindi cha Nitetee, Flora Lauo.

No comments: