Tuesday, March 20, 2018

RAIS MAGUFULI AKWAZIKA NA MAWAZIRI HAWA


RAIS John Magufuli amesema amekwazika kuona mawaziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba na wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina pamoja na makatibu wakuu wa wizara zao hawajahudhuria mkutano wa 11 wa Baraza la Biashara uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana.

Rais Magufuli alieleza kuchukizwa na watendaji hao wa serikali baada ya mmiliki wa viwanda cha maziwa mkoani Iringa, Fua Adrian, kueleza changamoto ya idadi ndogo ya viwanda vya maziwa nchini pamoja na kutokuwapo kwa sera kamili kwa viwanda vya maziwa nchini.

“Kwani kuna viwanda vingapi vya maziwa nchini? Waziri wa Mifugo naomba jibu, hayupo? Katibu Mkuu wake? Hayupo? Mtu yeyote aliyemwakilisha? Hakuna mtu? Haya basi Waziri wa Kilimo jibu kwa sababu inashabihiana... naye hayupo? Katibu wake? Hayupo? Mtu yeyote aliyemwakilisha? Hayupo?” Rais Magufuli alihoji.

“Waziri Mkuu kwani hukuwaalika hawa wote? Hiyo kwamba ninawachukia hawa mawaziri, lakini kiukweli wamenikwaza, nitajua cha kuwauliza, leo (jana) tunazungumza masuala ya maziwa, lakini mawaziri hawapo, makatibu wakuu hawapo, wala wakurugenzi,” alisema Rais Magufuli.

Katika majibu yake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema alitoa mwaliko kwa mawaziri wote wanaohusika na uwekezaji nchini wakiwamo wawili hao ambao alisisitiza mkutano huo unawahusu na walipaswa kuhudhuria.

No comments: