Wednesday, March 14, 2018

FEROUZ AELEZA KILICHOMPOTEZA KIMUZIKI

Image result for picha za ferooz
MUZIKI ni lugha inayozungumza na watu wengi. Inaweza kuwaweka watu chini, mataifa kwa mataifa hata yakasikilizana hata kama hayazungumzi lugha moja.

Tazama nyimbo kama Waving Flag ya K-Naan, Waka Waka ya Shakira na Coming Home ya Skylar Grey. Ni mfano wa nyimbo ambazo mtu yeyote, kutoka taifa lolote akisikiliza zinamgusa na hata kumuonyesha kitu kwenye maisha yake, cha kufanya au kuacha.

Hivyo ndivyo muziki ulivyo. Una nguvu sana. Ndiyo maana hata Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa alipomzawadia gari

mwanamuziki Feruzi Mrisho ‘Ferooz’, kutokana na Wimbo wa Starehe halikuwa tukio la kushangaza sana.

Lakini lilikuwa ni tukio la kumpongeza Ferooz kutokana na kazi yake hiyo nzuri aliyokuwa amefanya akimshirikisha Professor Jay.

Ferooz wakati wa ‘utawala’ wake alikuwa lulu. Ukiachana na kutamba akiwa chini ya Kundi la Daz Nundaz, na wanamuziki wenzake wakiwemo Daz Baba, Sajo na Lalumba, hata katika kazi zake mwenyewe alikuwa akifanya poa sana.

Chini ya Daz Nundaz, walifanya albamu moja iitwayo Kamanda na yeye mwenyewe alifanya albamu mbili ikiwemo Safari. Hata hivyo baada ya kutikisa sana baadaye kundi lake lilianza kutetereka hata kukosea mwelekeo na Ferooz, mwenyewe akapotea kabisa.

Baada ya kupotea mambo mengi yalisemwa juu yake na kundi lake kwamba walikuwa wamedumbukia kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Muda mwingi Ferooz amekuwa akipambana kurudi kwenye gemu kama ilivyo awali, lakini bado hajafika kule alikokuwa.

Katika makala haya, Ferooz anafunguka juu ya jitihada zake kwa sasa za kurudi kimuziki, nini anafanya na kazi zipi ameandaa kuweza kumrudisha kwenye kilele.

Risasi: Umekuwa ukijaribu kukomaa kurudi kwenye gemu, lakini bado hufiki kule ambako ulikuwa awali, nini tatizo?

Ferouz: Unajua kwanza muziki unabadilika. Siku hizi kuna mambo mengi unatakiwa kufanya katika muziki ili kuweza kuwa juu, si kama zamani. Na kikubwa pesa zinahitajika na hata menejimenti ya kusimamia kazi ni muhimu. Kwa hiyo kinachonifelisha ni kwamba sina menejimenti.

Risasi: Kupotea kwa Kundi la Daz Nundaz na wewe, kuna uhusiano wowote?

Ferouz: Hapana. Kumbuka Daz Nundaz ilikuwa inaundwa na watu. Sasa kupotea kwa watu siyo kwamba ndiyo ilikuwa ni sababu ya mimi kupotea. Kila mmoja alidondoka kwa wakati wake na changamoto zake.

Risasi: Vipi kuhusu dawa za kulevya, zinaweza kuwa chanzo cha kukupoteza?

Ferouz: Changamoto nilizozizungumza hapo juu ndiyo hasa zilizonifanya kudondoka

kimuziki. Mambo mengine ni ya ujana tu na kwa sasa ninachofanya ni kuhakikisha kazi yangu inasimama kama awali.

Risasi: Vipi lakini kuhusu Daz Nundaz, ndiyo limeshakufa au?

Ferouz: Ndiyo ni kama limekufa. Maana ukiangalia kila mtu anafanya mambo yake. Daz Baba anafanya yake, Sajo naye vilevile kila mmoja yupo bize kivyake. Kwa hiyo ni kama kundi halipo tena.

Risasi: Miongoni mwa kazi zilizokupa mafanikio makubwa ni ngoma ya 'Starehe', unaweza kuyaelezea kwa ufupi mafanikio iliyokupa?

Ferouz: Ndiyo ni ukweli kwamba wimbo wa Starehe ulifanya vizuri sana kwa upande wangu. Miongoni mwa mafanikio niliyoyapata ni shoo nyingi, zawadi
ya gari kutoka kwa Rais, wadau wa muziki wangu waliongezeka na mambo mengine mengi.

Risasi: Unaweza kuzungumzia ni katika mazingira gani hayo ambayo ulipewa usafiri huo, Rais mwenyewe ndiye alikupigia simu na kukwambia kwamba ana zawadi yako au ilikuwaje, na ilikuwa gari aina gani?

Ferouz: Masuala ya kiserikali huwa sipendi kuyazungumzia zaidi, lakini gari ilikuwa ni Jeep na ibaki ikieleweka hivyo tu.

Risasi: Tukizungumzia kwa sasa ni projekti gani ambazo unapanga kuziachia?

Ferouz: Nimeachia kazi zangu tayari mpya kwa sasa. Nakaza Roho na Jaribu, video zote nimefanya na Kilonzo. Lakini pia mashabiki wangu wategemee makubwa kwa sasa.

No comments: