Thursday, December 21, 2017

URAFIKI DAR YAWATIMUA WAPANGAJI WAKE


UONGOZI wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki cha jijini Dar es Salaam umetoa siku kwa wapangaji wake zaidi ya 160 kulipa malimbikizo ya pango la nyumba wanayodaiwa kabla ya kuwaondoa bila kujali hadhi zao na kupiga mnada mali zao kufidia madeni.

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi Desemba 21,2017 na naibu meneja wa kiwanda hicho, Shadrack Nsekela wakati akizungumza na waandishi wa habari leo. Amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya wapangaji kushindwa kulipa malimbikizo ya madeni wanayodaiwa tangu mwaka 2015.

“Tumeamua hatumhurumii mtu katika hili, wote tutawaondoa bila kujali hadhi zao. Tulianza kuwapa notisi tangu mwaka 2015, lakini mpaka sasa hawajalipa, tunawatoa wote,” alisema Nsekela.

Kwa mujibu wa Nsekela amesema wapangaji waliopo kota za Urafiki, Dar wanadaiwa pesa kati ya Sh. 600 milioni na Sh. 1 bilioni. Nsekela amesema wameanza kuwafukuza wapangaji wa ofisi, wakati wapangaji wa makazi wakitakiwa kujiandaa wakati wowote nao watatimuliwa.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono, Scholastika Kevela amesema baada ya siku 14 watapiga mnada mali walizokamata ili kufidia madeni hayo.  Amesema pia kuna yadi ya magari ambayo imefungwa huku wahusika wake wakishindwa kulipa, hivyo mnada utafanyika bila kuwaonea haya.

No comments: