Monday, October 9, 2017

WATATU KIZIMBANI DAR KWA MAUAJI YA MWANAHARAKATI


Ndugu wawili, Khalid na Rahma Mwinyi na Mohammed Maganga wamefikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa mauaji.

Washtakiwa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kumuua mwanaharakati wa kupinga ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo, Wayne Lotter.

Wakili wa Serikali, Adolf Mkini mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri amewasomea mashtaka leo Jumatatu.

Wanadaiwa Agosti 16 katika makutano ya barabara ya Chole na Haile Selasie wilayani Kinondoni walimuua kwa kumpiga risasi Lotter aliyekuwa akifanya kazi na kampuni ya Pams Foundation ya Arusha.

Baada ya kusomewa shtaka, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri la mauaji isipokuwa Mahakama Kuu.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi haujakamilika. Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 23 kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wamepelekwa rumande kwa sababu shtaka linalowakabili halina dhamana kisheria.

Wakati huohuo, Rahma Mwinyi, Mohammed Maganga na mwanafunzi, Almas Swed wamepandishwa kizimbani mahakamani hapo wakidaiwa kupatikana na silaha na risasi 167.

Wakili Mkini katika shtaka la kwanza amesema washtakiwa wanadaiwa Septemba 16, eneo la Upanga walikutwa wakiwa na bunduki aina ya Uzi na Rifle bila ya kuwa na kibali.

Washtakiwa katika shtaka la pili, wanadaiwa kupatikana na risasi 167 walizokuwa wakizimiliki bila kuwa na kibali.

Katika shtaka la tatu wanadaiwa walipatikana na bomu la kutupwa kwa mkono bila ya kuwa na mamlaka ya kuwa nalo.

Baada ya kusomewa mashtaka walikana kutenda makosa hayo. Upande wa mashtaka umedai upelelezi haujakamilika.

Wakili wa utetezi, Mluge Kaloli ameiomba Mahakama iwape dhamana wateja wake kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhaminika kisheria.

Hakimu Mashauri aliyekataa pingamizi la Jamhuri iliyodai Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana, amewataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho watakaosaini dhamana ya maneno ya Sh20 milioni.

Hata hivyo, ni Swed pekee anayepaswa kudhaminiwa kwa kuwa washtakiwa wenzake wanakabiliwa na kesi ya mauaji.

Swed alipelekwa rumande pamoja na wenzake kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi itatajwa Oktoba 23.

No comments: