Tuesday, October 3, 2017

SAID WA SCORPION KUFIKISHWA KORTINI

SAKATA la Said Mrisho aliyedaiwa kutobolewa macho na Salum Njwete ‘Scorpion’ na mkewe Stara Sudy, linatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kushindwa kuelewana ngazi ya Ustawi wa Jamii.

Said na mkewe waliingia kwenye mvutano mzito siku chache zilizopita baada ya kutengana na kufikishana Ustawi wa Jamii ambapo waliafikiana wagawane mali, lakini Said amekuwa akisuasua kufanya hivyo, jambo lililopelekea suala hilo kupelekwa mahakamani.

Chanzo chetu cha karibu kilieleza kuwa, licha ya kuwekeana makubaliano hayo mbele ya maofisa wa Ustawi wa Jamii kwamba Said ampe Stara pikipiki mbili na Bajaj moja, Said amekuwa akitoa visingizio vya hapa na pale na kushindwa kutimiza ahadi hiyo, jambo lililopelekea maofisa wa Ustawi waidhinishe kesi hiyo kusikilizwa mahakamani.

Gazeti la Uwazi lilimtafuta Stara ambaye alikiri ni kweli wanapaswa waende mahakamani, kwa sababu Said ameshindwa kutekeleza kile alichoahidi.
“Tangu tulivyokubaliana anipe sehemu ya mali hadi leo hajatimiza ahadi yake zaidi ya visingizio tu na kutupiga kalenda na kibaya zaidi kuna pesa ambayo alitakiwa anipe kwa siku kwa ajili ya kutunza watoto lakini nayo hatoi yote anatoa pungufu, ndiyo maana Ustawi wameona bora hili jambo liende mahakamani maana limewachosha,” alisema Stara.

Baada kuzungumza na Stara mwandishi wetu alimtafuta pia Said ambaye alikiri ni kweli bado hajampa Stara vitu hivyo kwa kuwa anashindwa kutekeleza matakwa yake ili na yeye nafsi yake iwe huru.

“Hivyo vitu nitampa lakini anashindwa kutekeleza masharti niliyompa, anatakiwa anipe hati ya kiwanja ambacho nilinunua kwa kaka yake, lakini hataki anasema watanirudishia pesa na wakati hiyo hati anayo.  Pia makaratasi yangu ya hospitali yeye ndiyo anayo hataki kunipa, sielewi sasa,” alisema Said.

TUJIKUMBUSHE
Kipindi kifupi cha nyuma Said na mkewe huyo aliyezaa naye watoto wanne aliingia kwenye mgogoro baada ya kijana huyo kumkimbia Stara akiwa na watoto wachanga mapacha na kwenda kuoa mke mwingine, ndipo sekeseke hilo likafika Ustawi wa Jamii na kuafikiana kugawana mali.

No comments: