Tuesday, October 3, 2017

MKAZI WA CHATO KORTINI KISUTI KWA KOSA LA MTANDAONI

Obadia Frank alipofikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, DSM.
MKAZI wa Chato mkoani Geita, Obadia Frank (41), mapema leo  amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.

Akisomewa  hati ya mashtaka na wakili wa serikali, Leonard Challo, amedai mshtakiwa huyo ambaye ni wakala wa Bayport ametenda  kosa hilo Agosti 8 mwaka huu, katika Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Imedaiwa mbele ya Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri, kuwa siku hiyo mshtakiwa alichapisha taarifa kupitia ukurasa wake wa Facebook uliokuwa ukihusiana na mazungumzo kati ya serikali na kampuni ya Acacia.

Imedaiwa mshitakiwa ametenda hayo huku akijua kuwa taarifa hizo ni uongo na zilikuwa na nia ya  kuipotosha jamii.

Hata hivyo mshtakiwa huyo anayetetewa na wakili Peter Kibatala, amekana kutenda kosa hilo na amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti na kesi hiyo itatajwa tena tarehe 16 Oktoba mwaka huu.


Mahakama imemtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao walitakiwa kuweka bondi ya Sh. milioni tano.

No comments: