Friday, October 6, 2017

KIMBUNGA NATE CHAWAUA WATU 20 AMERIKA YA KATI

Mvua kubwa imesababisha mito kufurika na kuathiri miji kote Costa Rica
Kimbunga Nate kimewaua watu zaidi ya 20 nchini Costa Rica, Nicaragua na Honduras huku kikielekea kaskazini upande wa Marekani.

Hali ya dharura imetangazwa katika mataifa kadha ya Amerika ya Kati ambapo watu zaidi ya 20 bado hawajulikani walipo.

Kimbunga hicho kimesababisha mvua kubwa, maporomoko ya ardhi na mafuriko.

Barabara nyingi hazipitiki, madaraja yameporomoka na pia kimesababisha uharibifu mkubwa kwenye nyumba za watu na majengo.

Nchini Costa Rica, watu karibu 400,000 hawana maji na maelfu wengine wameachwa bila makao na wanalala kwenye vyumba vya muda.

Watu zaidi ya sita wamethibitishwa kufariki katika taifa hilo.

Watu wengine 11 waliuawa kimbunga hicho kilipokuwa kinaelekea kaskazini na kufika Nicaragua.

Watu watatu wameuawa nchini Honduras na kuna watu kadha ambao hawajulikani waliko.
Nyumba zilizoharibiwa San Jose, Costa Rica Oktoba 5, 2017
Nchini Costa Rica, safari zote za treni zimesitishwa na safari kadha za ndege pia zimefutwa.

Mbuga kadha za taifa ambazo ni maarufu kwa watalii pia zimefungwa kama tahadhari.

Kimbunga hicho pia kimesababisha uharibifu mkubwa kwenye miundo mbinu Nicaragua.
Kimbunga

No comments: