Sunday, September 17, 2017

WATATU WAKAMATWA NA POLISI TIP-SINZA KISA MAOMBI YA LISSU

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Muliro Jumanne akiongea na wanahabari.
Watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni wanachama wa Chadema wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa kuhojiwa kuhusu mpango wa maombezi uliopangwa kufanyika katika uwanja wa Tip -Sinza, wilayani Ubungo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Muliro Jumanne aliyekuwa uwanjani hapo na kikosi cha askari zaidi ya 25 amesema watu hao walikamatwa saa 3:40 asubuhi wakiwa eneo hilo.
Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobasi Katambi akiongea na wanahabari.
 Amesema, “Atakayetaka kujaribu aje ila cha moto atakiona kwa sababu jitihada za kuzuia watu wema wasikanyage hapa zimeshafanyika sasa wanakuja kufuata nini.” Katika eneo hilo, polisi walikuwa wakiziondoa bajaji wakiwataka madereva wasiziegeshe hapo kwa siku ya leo.

Baadhi ya polisi wameonekana wakiwa na mabomu ya kutoa machozi na walifika uwanjani hapo wakiwa kwenye magari aina ya Toyota Land Cruiser.

Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo - Chadema  (Bavicha) jana Jumamosi lilitoa taarifa likisema leo litaungana na viongozi wa kiroho kufanya maombi maalumu kumwombea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeendelea na matibabu Nairobi, Kenya baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi mjini Dodoma tarehe 7 Septemba mwaka huu.

Viongozi wa Bavicha waliofika uwanjani hapo wamekimbia baada ya polisi kuwafuata walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari.
Angalia Video ya tukio hilo hapa chini:


No comments: