Tuesday, November 27, 2012

MSANII SHARO MILIONEA AFARIKI DUNIA

Marehemu Hussein Ramadhani Mkieti a.k.a. Sharo Milionea


Muigizaji, mchekeshaji na mwanamuziki Hussein Ramadhan Mkieti a.k.a. Sharo Milionea amefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Maguzoni Songa lililopo katika kijiji cha Lusanga wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Akithibitisha tukio hilo kupitia Clouds FM Radio kupitia kipindi cha Ala za roho kinachoendeshwa na mtangazaji Diva loveness love, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe  amesema kuwa marehemu Sharo amepata ajali majira ya saa 2.00 usiku akiwa peke yake anaendesha gari aina ya Toyota Harrier na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Muheza.

“Leo majira ya saa mbili usiku kwenye barabara ya Segera-Muheza mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Hussein Ramadhani au Sharo Milionea akiwa anaendesha gari namba T478 BVR Toyota Harrier akitokea Dar es salaam kwenda Muheza alipofika eneo la Maguzoni Songa wilayani Muheza hilo gari lake liliacha njia na kupinduka mara kadhaa na kusababisha kifo chake.  Mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali Teule ya wilaya ya Muheza”


Naye mama mkubwa wa marehemu, bi. Fatma Mkieti akiongea na Redio Clouds FM amethibitisha kutokea kwa kifo hicho...

"Tulipopata hizo habari tulienda hospitali ya wilaya ya Muheza kwenda kuhakikisha.  Hatukufanikiwa kuuona mwili bali daktari ametuonesha picha zake ndipo tukathibitisha kuwa ni kweli ni yeye Sharo Milionea ndiye aliyefariki.  Msiba upo nyumbani Lusanga, Muheza na kwa vile marehemu alikuwa ni mtu wa watu, familia imepanga azikwe siku ya Jumatano ili kuwapa nafasi waliopo mbali kuweza kuhudhuria mazishi yake," amesema.

Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Hussein Mkieti (Sharo Milionea). Amen.