Friday, April 13, 2012

VITABU VYA HISTORIA YA KANUMBA VYAUZWA MITAANI

Ikiwa ni siku tatu zimepita tangu aliyekuwa msanii nguli wa filamu nchini, Marehemu Steven Charles Kanumba azikwe tarehe 10 Aprili 2012, vitabu vya historia yake vimeanza kuonekana mitaani vikiuzwa.

Vitabu hivyo vinavyouzwa kwa bei ya Sh. 3,000/= vimeonekana sehemu mbalimbali ikiwemo maeneo ya mataa ya Ubungo ambapo mwandishi wa habari hii aliviona.

Haijajulikana mara moja kama vitabu hivyo vimetengenezwa na kuuzwa kwa idhini kutoka kwa ndugu wa marehemu au la, kufuatia tangazo lililotolewa leo katika vyombo vya habari na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya mazishi ya msanii huyo, ndugu Mtitu kwamba mtu yoyote hana ruhusa ya kutengeneza au kuuza kitu chochote kinachohusiana na marehemu Kanumba bila ya idhini kutoka kwa familia ya marehemu huyo.

Marehemu Steven Charles Kanumba alifariki ghafla usiku wa tarehe 7 Aprili 2012 nyumbani kwake Sinza Vatican baada ya kuanguka chumbani kwake akiwa na msanii mwenzie Elizabeth Michael, maarufu kwa jina la Lulu.

Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu. Amina.