Monday, January 16, 2012

REGIA MTEMA (MB) AFARIKI KATIKA AJALI


Marehemu Regia Mtema, enzi za uhai wake.





















Na Ipyana Mwaipaja
Aliyekuwa Mbunge viti maalum kwa tiketi ya chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Regia Mtema (32) amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Ruvu mkoani Pwani jana (14/01/2012) asubuhi.

 Katika gari hilo, marehemu aliambatana na abiria wengine saba ambao wote wamejeruhiwa.  Wawili kati yao hali zao ni mbaya na wamepelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam na wengine watano wamepelekwa katika Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha.

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, ameielezea ajali hiyo kuwa ilitokea baada ya marehemu ambaye ndiye alikuwa dereva wa gari hilo kulipita gari la mbele yake na kukutana na gari lingine likija mbele kwa kasi, hivyo alijaribu kukwepa na kufanya gari hilo kupinduka.

"Marehemu alijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake na ghafla aliona gari lingine likija kasi mbele yake,  katika kujaribu kulikwepa, ndipo gari hilo lilipinduka." alisema Mangu.


Taarifa iliyotolewa na Chadema imesema kuwa mipango ya mazishi ya marehemu inafanyika nyumbani kwa baba yake, Tabata, Dar es Salaam.

Mungu ailaze roho ya marehemu Regia Mtema mahali pema peponi, Amen. 


Gari ambalo marehemu Regia Mtema alipata nalo ajali jana asubuhi
maeneo ya Ruvu, mkoa wa Pwani likiwa limeegeshwa
katika kituo cha Polisi cha Mlandizi.